May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mpango: Sitovumilia atayebeza Muungano

Dk. Philip Mpango, Makamu wa Rais Tanzania

Spread the love

 

MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Dk. Phillip Mpango, amewaonya watu wanaobeza muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ulioasisiwa tarehe 26 Aprili 1964. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Dk. Mpango ametoa onyo hilo, leo Jumatatu tarehe 26 Aprili 2021, wakati akifungua Kongamano la Kuadhimisha Miaka 57 ya Muungano, jijini Dodoma.

Akizungumza katika kongamano hilo lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali na wananchi, Dk. Mpango amesema, katika kipindi chake cha Umakamu wa Rais wa Tanzania, hatokuwa mpole kwa watu watakaobeza muungano.

“Katika kipindi changu kama makamu wa rais sitakubali kabisa wanaochezea muungano wetu adhimu, kuna baadhi ya mambo huwa watu wanasema mimi ni mpole lakini kuna vitu nasema mimi sio mpole.”

“Nilishasema wabadhirifu wa mali za umma hapana, mimi si mpole, lakini naongeza tena watakaojaribu kuchezea muungano mimi sio mpole,” amesema Dk. Mpango.

Makamu huyo wa rais amesema, atashirikiana na Serikali ya Zanzibar, kuhakikisha muungano huo ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julisu Nyerere na Abeid Amani Karume unakuwa imara.

“Nitashirikiana na serikali za pande zote mbili na wananchi kuhakikisha muungano uanendelea kuwa imara paidi, pia nitahakikisha changamoto zilizobaki zinapatiwa ufumbuzi,” amesema Dk. Mpango.

Mwanasiasa huyo amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Nane ya Mapinduzi Zanzibar, chini ya Dk. Hussein Mwinyi, zimejidhatiti kuimarisha muungano huo.

“Hivyo serikali zote mbili zitaendelea kushirikiana kwa pamoja kuhuisha na kuboresha muungano, mtakumbuka kuwa kuweka suala la muungano chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais ni suala zuri kuhakikisha muungano unalindwa kama mboni ya jicho,” amesema Dk. Mpango.

error: Content is protected !!