MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango amewaagiza mawaziri watano kuelekea katika Bonde la Ihefu na kufanya tathmini ya uharibifu wa mazingira katika eneo hilo na kumpatia taarifa ya hatua walizochukua. Anaripoti Mwandishi Wetu….(endelea)
Mawaziri hao na wizara zao kwenye mabano ni Angela Mabula (ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, Juma Aweso (maji), Hussein Bashe (kilimo), Mashimba Ndaki (mifugo na uvuvi) na Dk. Damas Ndumbaro (maliasili na utalii). Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea)
Dk. Mpango ametoa maagizo hay oleo tarehe 12 Februari, 2022 wakati akizindua Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 katika Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Amewaagiza mawaziri hayo kutekeleza maelekezo hayo baada ya kikao cha Bunge kuhitimishwa.
Pia ameiagiza Kamati ya Bunge isimamie maagizo hayo kwani ni jambo lenye masilahi mapana kwa taifa.
Ametoa wito kwa wananchi na viongozi wa ngazi zote kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji
“Mfano chanzo cha mto Ruaha katika bonde la Ihefu, mawaziri hakikisheni kuna matumizi endelevu ya mto huo pamoja na mito mingine.
“Nafahamu baadhi ya viongozi wana makundi makubwa ya mifugo ndani ya bonde la Ihefu, wengine wawekezaji wakubwa wana mashamba makubwa ya mpunga na wanaelekeza maji kwenye mashamba yao kiholela bila utaratibu wa kuyarejesha mtoni,” amesema Dk. Mpango
Amesema hayupo tayari kuona ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere unakamilika lakini maji hayapatikani kutokana na uharibifu unaofanyika katika vyanzo vyote vya mto Rufiji.
Amesema shughuli za ufugaji ni muhimu lakini ni lazima zifanywe bila kuvunja hseria za uhifadhi wa mazingira.
Aidha, katika kuhakikisha jiji la Dodoma linakuwa safi, amemuagiza Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo kusimamia uundaji wa timu itakayokuwa chini ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, jiji la Dodoma, TFS na wadau wengine.
“Timu hiyo itayarishe mpango mkakati wa utekelezaji wa kusafisha mji wa Dodoma, na zoezi litakuwa endelevu, nataka nipate mpango huo ndani ya siku 30 kutoka leo…
nataka Dodoma iwe kama Singapore, lazima iwe ya kijani,” amesema.
Aidha, uniletee mpango kila baada ya miezi mitatu na utekelezaji ukilegalega wahusika wote wawajibike wenyewe kabla sijaingilia kati,” amesema.
Awali akizungumzia sera hiyo, Jafo amesema sera hiyo itaongeza fursa ya jinsi gani urejeshaji wa taka unaweza kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Pia suala la urejeshaji wa taka katika maendeleo na namna ya kutumia mbinu mbadala kuhakikisha taka zinarejeshwa.
“Sera itasaidia kupata bidhaa rafiki za mazingira mfano mifuko badala ya mifuko ya plastiki,” amesema.
Leave a comment