May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mpango atua Chato, azuru kaburi la Magufuli

Spread the love

 

MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, amewasili nyumbani kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Hayati John Pombe Magufuli, Chato mkoani Geita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Chato … (endelea).

Dk. Mpango, amewasili Uwanja wa Ndege wa Chato, leo Ijumaa, tarehe 14 Mei 2021 na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa Mkoa huo, akiwemo Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Robert Gabriel.

Mara baada ya kuwasili uwanjani hapo, msafara wa Dk. Mpango ulikwenda nyumbani kwa Hayati Magufuli na kupata fursa ya kuzuru kaburi lake.

Hayati Magufuli, alifikwa na mauti akiwa madarakani, saa 12:00 jioni ya tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, iliyopo Makumbusho, mkoani Dar es Salaam na mwili wake, kuzikwa nyumbani kwao, Chato 26 Machi 2021.

Dk. Mpango, amezuru kaburi hilo, akiwa njiani kwenda wilayani Kibondo, Mkoa wa Kigoma, kwa ajili ya kufunga kampeni za uchaguzi mdogo za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa ubunge jimbo la Muhambwe, utakaofanyika Jumapili hii tarehe 16 Mei 2021.

Pia, uchaguzi kama huo, unafanyika Jimbo la Buhigwe mkoani humo.

Uchaguzi wa Muhambwe, unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wake, Dk. Mpango kuteuliwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwa makamu wa Rais.

Ni baada ya Samia, aliyekuwa makamu wa Rais, kuapishwa kuwa Rais tarehe 19 Machi 2021, kuchukua nafasi ya Hayati Magufuli.

Huku uchaguzi wa Buhigwe, unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wake, Atashasta Nditiye, kufariki dunia katika ajali ya gari, tarehe 12 Februari 2021, jijini Dodoma.

error: Content is protected !!