MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango ametoa maelekezo saba kwa Wizara na taasisi mablimbali nchini katika kuhakikisha Kiswahili kinatumika ipasavyo katika shughuli mbalimbali za serikali. Anaripoti Jonas Mushi, Dar es Salaam … (endelea).
Ametoa maagizo hayo leo Alhamisi tarehe 7 Julai, 2022, katika sherehe za maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani zilizofanyika kitaifa jijini Dar es Salaam.
Dk. Mpango ameziagiza Wizara na taasisi za serikali kuendelea kutekeleza maagizo ya serikali yaliyokwisha kutolewa kwamba nyaraka za mawasiliano za wizara na idara zake ziwe kwa lugha ya Kiswahili. Pia mikutano, warsa, semina mijadala ya umma na dhifa ziendeshwe kwa Kiswahili.
Makamu huyo wa Rais pia ameagiza majina ya barabara mitaa, mabango fomu za usahili na maelekezo ya dawa zote na bidhaa na huduma ziandikwe kwa Kiswahili.
Mbali na hayo ameelekeza taarifa za miradi na mikataba inayohusu wananchi “lazima” iwe kwa Kiswahili “isiwe kwa lugha za kigeni pekee,” na kusema lengo ni kuhakikisha kila mwananchi anaelewa jambo linalohusu ustawi wa maisha yake.
Vilevile ameelekeza Sheria na kanuni ambazo bado hazijatafsiriwa zitafsiriwe na Wizara na Taasisi zinazosimamia sheria na kanuni hizo, kwa kushirikiana na mabaraza ya Kiswahili, wataalamu wengine wa Kiswahili na Ofisi ya Mwanasehria mkuu wa Serikali.
Pia ameagiza vyombo vya habari vinavyotumia Kiswahili “vihakikishe” vinatumia Kiswahili fasaha na sanifu, huku “vikizingatia kwa dhati” sarufi ya Kiswahili.
Aidha, pale anaposhirikishwa mtu anayeongea lugha isiyokuwa Kiswahili, ameelekeza chombo cha habari husika “kitoe tafsiri ya maneno yasiyo ya Kiswahili ili wananchi waelewe kinachozungumzwa.”
Dk. Mpango amesisitiza agizo lililotolewa na Rais Samia kwa balozi zote za Tanzania kuanzisha vituo vya kufunzia lugha ya Kiswahili.
“Na hapa napenda niagize balozi zote ziwatumie wataalamu wa Kiswahili walio sajiliwa kwenye kanzi data ya BAKITA na BAKIZA-Dk,” amesema Dk. Mpango.
Maelekezo mengine ni BAKITA na BAKIZA kuwa wabunifu katika kuzalisha misamiati ya Kiswahili ili kuendana na kasi ya maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia na Wizara na taasisi husika kuhakikisha mfumo wa kufundisha Kiswahili kwa wageni kwa njia ya mtandao Swahili Prime unatumika kikamilifu.
Leave a comment