May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mpango atoa maagizo kwa Mwigulu, Jafo

Dk Philip Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Spread the love

 

MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Dk. Phillip Mpango, amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, kuongeza mapato ya nchi kutoka wastani wa Sh.1 trilioni hadi Sh. 2 trilioni kwa mwezi, ifikapo mwishoni mwa 2021. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Dk. Mpango amempa maagizo hayo Dk. Mwigulu leo Alhamisi tarehe 1 Aprili 2021, baada ya mwanasiasa huyo, kuapishwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Dk. Mwigulu pamoja na viongozi wengine 16, akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga, mawaziri nane na manaibu waziri nane, walioteuliwa jana Jumatano na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wameapishwa leo jijini Dodoma.

“Wizara zote ni lazima zisimamie mapato, Dk. Mwigulu upande ule wa kodi, lakini pia mapato kutoka taasisi zetu na mashirika bado bado sana.”

“Tunataka kuona mapato yanaongezeka na zamu hii ningependa waziri wa fedha kabla ya mwisho wa mwaka huu, tuwe tumefikia wastani wa Sh.2 trilioni kwa mwezi, inawezekana mkajipange vizuri,” ameagiza Dk. Mpango.

Mbali na kibarua cha kuongeza mapato ya nchi, Dk. Mpango amemuagiza Dk. Mwigulu kwa kushirikiana na Waziri Ofisi Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, Seleman Jafo, kutatua mara moja changomoto ya masuala ya fedha katika muungano.

“Nashukuru nimepata mrithi Dk. Mwigulu, hii ndio iwe kazi yako ya kwanza, msaidiane na naibu waziri na timu nzima lakini pia sasa Waziri Jafo iwe kazi ya kwanza kuhakikisha kwamba tunatatua hilo tatizo haraka iwezekanavyo,” ameagiza Dk. Mpango.

Dk. Philip Mpango, Makamu wa Rais wa Tanzania akiapa

Makamu huyo wa Rais ametoa agizo hilo, siku moja baada ya Rais Samia kumuagiza akaimalize changamoto hiyo.

“Jana nilikaa mpaka saa 12 na hasa nikitafakari agizo lako (Rais Samia) kwamba, sasa huyu mchawi ambaye anakuwa anashindwa kutatua masuala ya mahusiano ya kifedha katika pande zetu mbili za muungano, sasa nimepewa huyo mtoto nifanye hiyo kazi,” amesema Dk. Mpango

Vilevile, Dk. Mpango amewaagiza mawaziri wote hasa Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ummy Mwalimu, kusimamia ukusanyaji wa maduhuli pamoja na kudhibiti matumizi ya fedha.

“Tamisemi huko kuna kazi kubwa, kuna kazi ya mapato na matumizi. Hayo mkasimamie katika wizara zote, mkusanye maduhuli vizuri na kuisimamia matumizi wizara zenu bila kupepesa macho, ikishindikana nitarudi kwa mama kumwambia huyu nafikiri hatoshi kuungana na sisi,” amesema Dk. Mpango.

error: Content is protected !!