October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mpango ampa mitihani minne Profesa Kitila

Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango

Spread the love

 

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango amemuagiza Waziri ya viwanda na biashara, Prof. Kitila Mkumbo pamoja na Shirikisho la wenye Viwanda nchini (CTI) kukaa mezani na kuja na majibu sahihi kuhusu maswali manne yanayodaiwa kukwamisha ukuaji wa sekta ya viwanda nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Maswali hayo manne yametolewa na Dk. Mpango leo tarehe 8 Oktoba 2021 wakati akizungumza katika hafla ya utoaji tuzo kwa wazalishaji bora wa viwanda kwa mwaka 2020.

Amesema licha ya umuhimu wa viwanda, bidhaa zinazotengenezwa na viwanda nchini hazikidhi mahitaji ya wananchi na soko la nje hali inayosababisha kuagiza bidhaa nyingi kutoka nje.

“Kwa mfano mwaka 2020 tumetumia bilioni 200 kuagiza bidhaa za vitambaa wakati pamba inazalishwa kwa wingi nchini, tumetumia Sh bilioni 111 kuagiza bidhaa za sabuni, Sh bilioni 93 kuagiza mafuta ghafi ya mawese, Sh bilioni 33 kuagiza bia zinazotokana na kimea japo tunalima ngano, mahindi na shayiri na Sh bilioni 29 kuagiza chumvi licha ya kuwa inazalishwa kwenye ukanda wa bahari,” amesema

Kutokana na hali hiyo ameiagiza wizara hiyo pamoja na CTI kufanya tafakuri ya kina na kuna na majibu sahihi kwa kuwa yeye na Rais Samia hawataki majibu mepesi.

Prof. Kitila Mkumbo

“Bado najiuliza maswali hivi kweli inatokana na kasi ndogo ya kutekeleza blue print? Kama ndivyo mbona baadhi ya bidhaa kama gypsam, saruji, ceramic nondo na platsick uzalishaji wake ni mzuri na wamejipenyeza kwa kasi katika masoko ya nje?. Tunatakiwa tutekeleze blue print kwa kiasi gani ili tuone badiliko kubwa zaidi katika uzalishaji kwenye viwanda vyetu?

“Swali la pili, Je, kasi ndogo ya uzalishaji bidhaa viwandani hususani sukari, mafuta ya kula nk. inatokana na uzalishaji mdogo malighafi viwandani au hususani zile zinazotokana na kilimo?

“Swali la tatu, Je, bidha za viwanda vyetu zinashindwa kushindana na bidhaa kutoka nje kwa sababu ya gharama kubwa uzalishaji kwa kuwa na gharama kubwa za nishati na miundombinu mingine?

“Swali la nne, Je, ni tatizo la ukosefu wa teknolojia au mitaji? Na kwa mabenki au taasisi za fedha hivi ni ngapi zinafuata na kuiga mfano wa CRDB katika kuwakopesha na kuwapa mitaji wamiliki wa viwanda iwe kwa gharama nafuu?,” amehoji.

Pamoja na hayo amesema yapo maswali mengi ila kwa sasa yafanyiwe kazi hayo ili kufikia malengo yaliyowekwa kwenye mpango wa tatu wa miaka mitano.

Awali Mwenyekiti wa CTI, Paul Makanza ameishukuru serikali kwa kuzipatia ufumbuzi baadhi ya changamoto ikiwamo suala la ukusanyaji wa kodi bila vitisho hali iliyochangia TRA kuongeza mapato kwa asilimia 17 kwa kipindi cha miezi mitatu.

Pamoja na hayo amesema bado wenye viwanda wanakabiliwa na changamoto kubwa ya mabadiliko ya sera na kanuni za uendeshaji wa biashara bila kushirikishwa.

“Lakini pia gharama kubwa za tozo za Tasac na ucheleweshaji wa utoaji mzigo bandarini bado ni kikwazo. Tunaomba kazi hii ifanywe na sekta binafsi,” amesema.

error: Content is protected !!