SPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson amemuagiza Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel kujibu tena swali la msingi na maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Viti Maalumu, Agnes Hokororo (CCM), baada ya kutoa majibu yasiyo sahihi kulingana na maswali hayo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma …(endelea).
Hii ni mara ya nne kwa Spika wa Bunge kuagiza mawaziri na manaibu wao kujibu maswali kwa usahihi katika Bunge la 12 Mkutano wa saba.
Mbali na Dk. Mollel, manaibu wengine waliobainika kutoa majibu yasiyo sahihi kwa nyakati tofauti bungeni ni Omary Kipanga (Elimu, Sayansi na Teknolojia), Patrobas Katambi (Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu) na Mhandisi Godfrey Msongwe (Ujenzi na Uchukuzi).
Aidha, akizungumza bungeni leo tarehe 26 Mei, 2022 jijini Dodoma baada ya kipindi maswali na majibu, Spika Tulia amesema jana katika kikao cha 30 cha Mkutano wa Saba wa Bunge hilo la Bajeti, Hokoro aliomba mwongozo wa Spika chini ya kanuni ya 76 ya kanuni za Kudumu za Bunge za mwaka 2020.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Hokororo kuuliza swali la msingi 267 kuhusu utoaji na upatikanaji wa huduma za afya ambalo liliekezwa kwa wizara ya afya na kujibiwa na Naibu Waziri kwa niaba ya Waziri wa afya.
Katika swali la pili la nyongeza, Hokororo alihoji je, ni sheria ipi kati ya sheria 30 inayosimamia wanawake na wajawazitio wakati wa kujifungua wanapopata huduma zisizoridhisha?
Je, sheria hizo zinaruhusu malipo ya fidia kwa wagonjwa wanaopata huduma zisizoridhisha au zisizo na ubora zinazopelekea athari za kiafya au hata kifo?
Akisoma majibu ya Naibu Waziri, Spika Tulia alisema,“ni kweli kumekuwapo na mambo anayosema kwa namna ya huduma ya mama na mtoto, lakini si tu sheria za nchi yetu bali pia taratibu za nchi yetu na kanuni za wizara ya afya zinataka mama mjamzito na mtoto wa chini ya miaka mitano wapate huduma bure.
“Lakini sasa tunapokuja kujibiwa vibaya kwa masuala ya fedheha maana yake kuna sheria za kiutumishi ambazo zipo zimeonesha watu wanaofanya mambo yanayofanana na hayo lakini kuna sheria za maadili ya kitaaluma ambayo mara nyingi anapopatatikana mtu ambaye amekuwa akijibu vibaya akifanya nini… wakati mwingine anapitishwa kwanza kwenye sheria za maadili ya kitaaluma, anawajibika lakini anaachiwa vilevile sheria za kiutumishi zichukue mkondo wake.
“Mbunge kama mdau mkubwa kwenye eneo hilo endelea kutusaidia na kutusaidia kutengeneza ushahidi wa kutosha kuwapata watu wa namna hiyo ili washughulikiwa kulingana na taratibu na sheria,” Spika Tulia alimaliza kusoma majibu ya Dk. Mollel.
Aidha, Spika Tulia amesema kutokana na majibu hayo, Hokororo aliomba muongozo wa Spika kuwa haelewi ni majibu ya swali namba moja au namba mbili, pia akataka kujua kama inaruhusiwa kwa Waziri kutojibu maswali na kusema atatoa majibu baadae?

Spika Tulia amesema alipitia taarifa za bunge na kubaini kuwa kweli swali halikujibiwa kikamilifu.
“Kwa sababu majibu ya maswali hayo hayaoneshi ni sheria ipi inayosimamia wanawake wajawazito wanaopata huduma zisizoridhisha wakati wa kujifungua na kama sheria hizo zinaruhusu malipo ya fidia kwa wagonjwa wanaopata huduma zisizoridhisha au zisizo na ubora.
“Majibu yaliyotolewa hayaeleweki ni ya swali la kwanza au la pili. Kwa kuwa Hokororo alitaka kujua hili linaruhusiwa au haliruhusiwi, namfahamisha jambo hilo haliruhusiwi na Naibu Waziri alipaswa kutoa majibu ya maswali hayo kwa ukamilifu,” amesema.
Amesema kwa kuzingatia masharti ya kanuni ya 53 ya kanuni za kudumu za Bunge za mwaka 2020 anaelekeza swali hilo lipatiwe majibu sahihi kama alivyoyahitaji mbunge huyo wa viti maalumu mkoa wa Mtwara.
Leave a comment