September 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mkumbo aibana Serikali kulipa fidia wanaopisha mradi wa mwendokasi

Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo,

Spread the love

MBUNGE wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo, ameitaka Serikali iwaruhusu wananchi 90 wa Ubungo Kiswani, waendelee na shughuli zao kama kawaida, baada ya kuchelewa kuwalipa fidia ya majengo yao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo kasi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Prof. Mkumbo ameyasema hayo wakati akiuliza swali bungeni jijini Dodoma, leo Alhamisi, tarehe 22 Septemba 2022.

Aidha, Prof. Mkumbo amesema suala hilo lina mgogoro kutokana kwamba wananchi hawakuridhika na viwango vya uthamini vilivyotolewa na mthamini mkuu wa Serikali.

“Waziri wa nchi ofisi ya Rais alifika katika mtaa wa Ubungo Kisiwani, tarehe 14 Mei 2022 na akafanya mkutano na wananchi pale na kulikuwa na mgogoro wa kiwango, aliagiza wataalamu wafanye tathimini ili warudi kwa wananchi waelewane kuhusu kiwango ambacho kinastahili. Lini hiyo ripoti itapatikana,” amesema Prof. Mkumbo na kuongeza:

“Kwa kuwa muda mrefu umepita wananchi hakuna kinachofanyika, hata anuani za makazi hazijafanyika kutokana na shughuli hii kwa nini Serikali kupitia naibu waziri mkatoa tamko kwamba kwa sababu fidia hii haijulikani italipwa lini, wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida.”

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais –TAMISEMI, David Silinde, amesema bado Serikali inahitaji kulitumia eneo hilo, na kwamba inatafuta hela kwa ajili ya kulipa fidia.

“Tutarudi kukaa na wananchi kueleza haya yote yanayoendelea, nimuondoe hofu kwamba kauli ya Serikali bado tunahitaji kuendelea kulitumia lile eneo ndiyo maana tunatafuta fedha kuwalipa kwa wakati na kama muda ukapita maana yake kuna nafasi mbili kwenye sheria, moja kurudia uthamini au kuwa na riba ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata fidia stahili kutokana na eneo lao,” amesema Silinde.

error: Content is protected !!