July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Migiro awekwa kitimoto bungeni

Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha- Rose Migiro,

Spread the love

WAZIRI wa Katiba na Sheria na Katiba, Dk. Asha Rose Migiro, jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya wabunge wa upinzani kuhoji juu ya Muswada wa Sheria ya kulinda watoa taarifa za Uhalifu na Mashahidi wa mwaka 2015.

Wabunge walieleza kuwa muswada huo umewahishwa kuwasilishwa bungeni bila kuwapo maandalizi ya kutosha. Dany Tibason anaripoti kutoka Dodoma … (endelea).

Dk. Migiro alikutana na kimbuga cha upinzani ikiwa ni siku moja baada ya wabunge kugomea serikali kuingiza bungeni miswada mitatu iliyowasilishwa na wizara ya nishati na madini.

Miswada ambayo ilikataliwa na wabunge kwa maelezo kwamba inahitaji muda mzuri, ni muswada usimamizi wa mapato ya mafuta na gesi; muswada wa kuhusu uwazi na uwajibikaji katika taasisi za uchimbaji na muswada wa sheria ya petrol.

Dk. Migiro alitaka Bunge lijadili na kuupitisha muswada huo ili kutoa nafasi ya kuwalinda watu wa aina hiyo.

Akiwasilisha maoni ya upinzani bungeni, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema, muswada huo hauna tija kwa muda huo kwani unatoa nafasi finyu kwa wabunge kujadili jambo ambalo ni muhimu zaidi kwa wananchi.

Alisema uharaka wa muswada huo, ni kiashiria tosha kwamba Serikali ilitaka kuminya uhuru wa wabunge kupitia kwa kina sheria hiyo.

Alisema, Kanuni zinasema, sheria inaweza kupitishwa kwa hati ya dharura ikiwa tu kuna mambo ambayo yanataka kutokea ambayo ni pamoja na majanga au vita.

Akahoji: “Katika hili, kuna uharaka kiasi gani wa kupitisha muswada huu?”

Mbali na kutoa ufafanuzi katika vifungu vingi katika muswada huo, Lissu alisisitiza kuwa ikiwa muswada huo utapitishwa na kuwa sheria, utakuwa umewanyima haki watu wa kada ya chini na kuwapa mwanya viongozi wao.

Naye mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alipinga vikali muswada huo pamoja na namna ulivyowasilishwa; jambo ambalo lilizua zogo kubwa kati yake na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju.

Malumbano kati ya Masaju na Mnyika yalianzia pale mbunge huyo machachari, aliposema kuwa serikali ni dhaifu katika suala zima la utungaji wa sheria.

Katika hoja zake, Mnyika alipinga jinsi muswada ulivyokuwa ukitoa upenyo kwa watu kutoa taarifa kwa wakubwa wao badala ya kuzipeleka taarifa hizo kwa vyombo vingine.

Mnyika alisema, muswada unaelekeza mtu kutoa taarifa kwa kiongozi wake na kuhoji, “mfanyakazi wa benki kuu anawezaje kutoa taarifa za ufisadi wa gavana kwa gavana mwenyewe?”

Mwanasheria alipinga kauli za kuwa Serikali inafanya vitu dhaifu akisema kuwa sio nia yao bali wanafanya kazi ya kupeleka miswada ili wabunge wenyewe ndiyo wafanye maamuzi.

Akichangia mjadala huo, mbunge wa Kigoma, Kusini David Kafulila, alipinga mfumo ambao unatumiwa katika kutengeneza sheria ya kuwalinda watoa taarifa kwa maelezo kuwa hauna maana yoyote.

Kafulila ambaye alitangaza kuwa yeye ni miongoni mwa wahangaalisema, ndani ya Tanzania kuna vitu vingi ambavyo vinafanywa ikiwemo ufisadi mkubwa unaowahusisha watu wa ngazi ya juu lakini hakuna wa kuwalinda.

Akiongea huku akimtolea macho Spika wa Bunge, Anne Makinda, Kafulila alisema, “Mimi nilipotoa taarifa humu ndani, kwanza spika ulisema nilichokoza mwenyewe. Nikaenda kwa RCO (Ofisa Upelelezi) mkoa wa Dodoma kisha kwa IGP, lakini kote sikupata msaada wowote.”

Aliongeza, “Kutokana na hilo, nikaamua kukimbilia Israel na kwenda kupiga magoti katika ukuta wa Suleiman ili nipate ulinzi ambao hadi leo ndiyo nategemea.”

Mbunge huyo alikumbushia suala la waandishi kulindwa katika kutoa na kuandika taarifa za uchunguzi. Alimtolea mfano mwandishi wa habari, Edson Kamukala ambaye kifo chake kimesheni utata.

Kwa upande wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Maria Hewa, ndiye aliyekuwa mbunge pekee aliyesema muswada huo ulikuwa na uharaka ambao haukutakiwa kwa wakati huo.

Wabunge wengine wa CCM waliochangia, ni Ismail Rage, Grace Puja na Dk. Mary Mwanjelwa. Wote waliunga mkono muswada huo.

Wengine waliochangia ni Davi Silinde (Chadema), ambaye alisema kuna masuala ya ubambikiziaji wa kesi na akataka serikali itenge muda wa kuangalia muswada kwa manufaa ya wengi kuliko ilivyo sasa.

error: Content is protected !!