April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mengi avunja rekodi ya mapokezi nchini

Spread the love

MAELFU ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro na mkoa jirani wa Arusha, wamejitokeza kuupokea mwili wa aliyekuwa mwenyekiti wa makampuni ya IPP Limited, Dk. Reginald Abraham Mengi. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Hai, Kilimanjaro … (endelea).

Mfanyabiashara huyo mashuhuri nchini na katika eneo zima la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, alikutwa na mauti usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita, tarehe 2 Mei 2019, akiwa jijini Dubai, Falme za Nchi za Kiarabu.

Taarifa zinasema, Dk. Mengi amefariki dunia kutokana na maradhi ya shinikizo la damu. Alikwenda katika eneo hilo la nchi za Falme za Kiarabu, kwa ajili ya mapumziko ya sikukuu ya Pasaka.

Kutoka uwanja wa ndege ya Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), hadi nyumbani kwake Machame – karibu na lango kuu la kuingia Mlima Kilimanjaro – maelfu ya wananchi wamejipanga barabarani kuupokea mwili wa Dk. Mengi.

Mwili wa Dk. Mengi, ulifikishwa mkoani Kilimanjaro kwa kutumia ndege ya kampuni binafsi ya Precision asubuhi ya leo tarehe 8 Mei 2019. Dk. Mengi anatarajiwa kuzikwa kesho kijijini kwake Machame.

Mwandishi wa habari na mmili wa Radio ya ABM, Abdallah Majura, ameeleza kuwa ameshindwa kufika nyumbani kwa Dk. Mengi kutoa salamu za pole na kupata nafasi ya kumuaga kutokana na jinsi watu walivyokuwa wengi.

“Tumeamua kurudi mjini na kusubiri kutoa heshima zetu kwa marehemu kesho, wakati mwili wake utakapofikishwa kanisani hapa Moshi. Watu wamejitokeza kwa wingi barabarani, huku wakiwa wamebeba majani ya miti na migomba mikononi mwao,” ameeleza.

Anasema, “Mzee huyu atakayemlipa fadhila zake, ni Mungu pekee. Hii haijawahi kutokea, kwamba masikini anazikwa na masikini wenzake,” ameeleza Saed Kubenea, mbunge wa Ubungo jijini Dar es Salaam, ambaye alikuwa mmoja wa marafiki wa karibu na Dk. Mengi.

Amesema, “pamoja na utajiri wake, Dk. Mengi aliishi kama mtu wa kawaida. Hakuwa na ulinzi. Mwenyewe alinieleza, ‘ninalindwa na Mungu.’ Nyumbani kwake na ofisini kwake, kulikuwa wazi kwa watu wote.”

Kubenea ambaye pia ni mwanahabari amekuwa akimuelezea Dk. Mengi kama mzazi, kaka, rafiki na kiongozi kwake. Anasema, alimchukua mithili ya mtoto wake wa kumzaa.

Akizungumza kwenye hafla ya kumuaga jana Jumanne zilizofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijiji Dar es Salaam, Kubenea alisema, hatasahau msaada wa Dk. Mengi kwake.

“Mwaka 2008 nilipopatwa na majanga mbalimbali ikiwemo lile la kumwagiwa acid, Mzee Mengi alijitolea kwa hali na mali kunifariji na kuhakikisha kuwa napata matibabu nje ya nchi bila ya kujali gharama zake,” alieleza na kuzusha huzuni kwa waombelezaji.

Alisema, “binafsi nimepata pigo kubwa. Nimeondokewa. Ni kweli kuwa watu wanasema, mlango mmoja ukifungwa, hufunguka mwingine, lakini ni ukweli uliowazi, kwamba hakuna Mengi wawili. Alikuwapo mmoja, naye ni Reginald Abraham Mengi, ambaye ndiye huyu aliyelala mahali hapa.”

Anasema, Dk. Mengi alikuwa mstari wa mbele kusaidia kila aliyekuwa na uhitaji. Yeye binafsi alimsaidia kukuza gazeti lake la MwanaHALISI bila ya kujali kuwa naye ni mmiliki wa magazeti ambayo ni wazi yalikuwa yakishindania soko moja.

Kuhusu uwanachama wake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kubenea anasema, hakuna uhakika kama Dk. Mengi alikuwa kweli mwanachama wa dhati wa chama hicho.

“Kwake, hizi itikadi zenu, lilikuwa siyo jambo muhimu. Lililokuwa muhimu, ni ajenda ya nchi na maendeleo ya watu. Milango yake ilikuwa wazi kwa watu wa itikadi zote na kwamba yeye alithamini utu wa mtu kuliko itikadi za vyama,” ameeleza Kubenea.

Anasema, “Dk. Mengi aliweza kutumia rasimali zake kusukuma ajenda ya maendeleo ya nchi, bila kujali nani amebeba ajenda hiyo. Alitumia fedha zake kusaidia vyama vyote. Ofisini yake pale Haidar Plaza na nyumbani kwake, walikutana watu wa itikadi tofauti.

“Hivyo basi, kama tunataka kumuenzi Dk. Mengi kwa dhati, ni muhimu kuiga hiyo spiriti. Tusijifanye tunampenda sana ndugu Mengi, wakati tunabaguana kwa itikadi zetu.”

Kubenea anasema, kuthibitisho hilo, katika uchaguzi mkuu uliyopita, ilani za vyama vyote vikubwa – CCM na UKAWA – ziliandaliwa nyumbani kwa Dk. Megi; na au kusheheni mawazo yake.

Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi iliyotolewa na familia ya marehemu Dk. Mengi, ibada ya mazishi itafanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania, mjini Moshi.

error: Content is protected !!