June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mashinji azindua Ofisi ya Chadema Kinondoni

Spread the love

Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameendelea na ziara zake za uimarishaji wa chama hicho kwa kufungua ofisi pamoja na matawi mbalimbali, anaandika Charles William.

Baada ya kufanya ziara ya kukagua uhai wa chama, kuzindua matawi na kuchangisha zaidi ya Sh. 12 milioni kwaajili ya ujenzi wa ofisi za Chadema Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani mwishoni mwa wiki iliyopita, siku ya leo Dk. Mashinji amezindua ofisi mpya za Chadema mkoa wa kichama wa Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Shughuli hiyo imefanyika katika Kata ya Makumbusho na kuhudhuriwa na wabunge, madiwani, wanachama na wapenzi wa chama hicho.

Miongoni mwa waliohudhuria uzinduzi wa ofisi hiyo ni pamoja na Suzan Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, Rose-Moshi Makey, diwani wa viti maalum, Henry Kilewo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kinondoni na Mhandisi Mustafa Muro ambaye ni mgombea umeya katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kupitia chama hicho.

Jumamosi ya wiki iliyopita, Dk. Mashinji aliueleza mtandao huu kuwa Chadema ipo katika mikakati ya kuhakikisha inakuwa na ofisi za uhakika kila kona ya nchi ikiwemo kujenga ofisi zake za kudumu kupitia michango ya wanachama wake.

“Sisi hatuna rasilimali za kutosha kuweza kujenga ofisi katika majimbo, wilaya na mikoa yote ndani ya muda mfupi, lakini tuna mtaji wa watu wanaokipenda chama hiki, kwahiyo tutautumia mtaji huo kuhakikisha tunajenga ofisi za chama katika maeneo mbalimbali kama lilivyoagiza Baraza Kuu la chama,” alisema.

error: Content is protected !!