August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Masaburi atutoka

Spread the love

DK. Didas Masaburi, aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, amefariki dunia jana saa 3:30 usiku kwa shinikizo la damu, anaandika Faki Sosi.

Dk. Masaburi alifariki akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya kulazwa kwa siku tano kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na ndugu zake wa karibu na kwamba, tayari mipango mbalimbali ya kusimamia mazishi yake inaendelea kupangwa.

Dk. Masaburi aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na pia mgombea Ubunge katika Jimbo la Ubungo kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kupitia Chama Cha Mapinduzi na kupata kura 59,514 dhidi ya Saed Kubenea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyepata kura 87,666.

Hata hivyo, baada ya matokeo hayo, Dk. Masaburi hakukubaliana nayo na kuamua kupeleka malalamiko yake mahakamani kupinga kushindwa na Kubenea, baadaye alifuta kesi hiyo.

Miongoni mwa kazi alizofanya Dk. Masaburi ndani ya CCM ni pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVICCM) kwa Mkoa wa Dar es Salaam mwaka 1995.

Mwaka 2010 Dk. Masaburi alichaguliwa kuwa Diwani wa Kata ya Kivukoni ambapo tarehe 23 Desemba mwaka huo, alichaguliwa kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Kabla ya mauti yake Dk. Masaburi alipelekwa India mara mbili kwa ajili ya matibabu lakini pia alikuwa akiishi na figo moja tangu mwaka 2000.

error: Content is protected !!