October 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Maryrose: Siwahofii Lissu, Msigwa urais Chadema

Dk. Maryrose Majinge, kada wa Chadema aliyetangaza nia ya kuwania Urais kupitia chama hicho

Spread the love

DAKTARI Maryrose Majinge, aliyejitokeza katika kinyang’anyiro cha kuomba kuteuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kugombea Urais wa Tanzania kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 amesema, haogopi vigogo atakaochuana nao katika mchakato huo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Dk. Majinge ametoa kauli hiyo leo Jumatatu tarehe 8 Juni 2020, alipoulizwa na MwanaHALISI ONLINE kwa simu, amejipangaje kukabiliana na ushindani kutoka kwa vigogo wa Chadema, waliotangaza hadharani nia ya kushiriki katika kinyang’anyiro hicho.

“Sina mashaka sababu, binafsi mimi ni mgombea mzuri, bila shaka nitapitishwa sababu chama kinaangalia mtu wa uhakika atakayekivusha, mtu aliyejiandaa na anayeweza. Chadema  kinaamini katika mabadiliko, “ amesema Dk. Majinge.

Tangu Chadema ifungue milango kwa wanachama wake wenye nia ya kutaka kugombea urais kupitia chama hicho, tarehe 3 hadi 15 Juni 2020, makada kadhaa wa wametangaza kujitosa katika mchakato huo.

Baadhi yao ni Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti Chadema, na Peter Msigwa, Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Nyasa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini.

Katika mchakato huo, Lissu amekuwa akipigiwa chapuo kubwa na baadhi ya wanasiasa kutoka ndani na nje ya Chadema, wakidai anatosha kuipeperusha bendera ya chama hicho, kwenye uchaguzi wa urais.

Lakini Dk. Majinge amesema, vuguvugu hilo halimuogopeshi, kwa kuwa amejipanga na anaamini ana sifa za kuteuliwa.

“Unapokuwa kiongozi, kuogopa huwa hakupo kwangu, hivyo kitu uoga ondoa. Kuhusu makada hao kujitokeza, nafarijika sababu raha ya ushindani ni kushindana, huwezi kwenda kwenye ushindani peke yako, yaani hainogi,” amesema Dk. Majinge.

“Nimefarijika  sana kwa hilo, na nichukue fursa hii kuwapongeza na kuhamasisha wengine wanaohisi wanatosha waingie, si unajua chama chetu ni cha demokrasia, hivyo hilo litathibitisha demokrasia,” amesisitiza

Dk. Majinge amesema, ili Chadema kipate mgombea mzuri, inatakiwa wanachama wengi wenye sifa na vigezo wajitokeze, ili uwepo ushindani utakaokisaidia kupata mgombea bora.

“Tunapokuwa wengi na wale wanaojiamini, mwisho wa siku tutampata wa uhakika na wa ukweli, nafurahia wamejitokeza kama hao,” amesema Dk. Majinge.

Dk. Majinge amesema, yuko tayari kwa uamuzi wowote, ingawa bado anaamini ana sifa za kushinda kwenye mchakato huo.

“Kama nilivyosema, najiamini niko vizuri, lakini katika vigezo hasa  ikionekana kuna mwingine mwenye vigezo vya kutosha kuliko mimi, unajua mashindano kuna matokeo ya aina mbili, kuna kushinda na kushindwa na vyote ni haki. Lakini ninachoombea ni haki itendeke mwisho wa siku tumpate mgombea bora,” amesema Dk. Majinge.

Mwaka 2015 Dk. Majinge  alijitosa katika mchakato wa uteuzi wa mgombea ubunge wa Ukonga ndani ya Chadema, lakini hakuteuliwa ambao Mwita Waitara, alipenya katika kinyang’anyiro hicho, na kufanikiwa kupeperusha bendera ya Chadema katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015.

Katika uchaguzi huo, Waitara alishinda kupitia Chadema, lakini baadae aliondoka katika chama hicho, kisha kugombea tena jimbo hilo katika uchaguzi mdogo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), na kufanikiwa shinda.

Baada ya ushindi huo, Rais wa Tanzania, John Magufuli, alimteua kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

error: Content is protected !!