August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mahanga: Nini kimempata Lembeli?

Spread the love

JAMES Lembeli amesikitisha wengi. Kauli yake ya kumshabikia Rais John Magufuli imeibua mjadala mkubwa, anaandika Charles William.

Lembeli aliibuka katika mkutano wa hadhara wa Rais Magufuli na wananchi wa Kahama mkoani Shinyanga na kusema;

“Nipo hapa kwasababu kazi unayoifanya sasa hivi mheshimiwa rais, ndiyo kazi ambayo kwa miaka 10 nikiwa mbunge niliipigania, lakini siwezi kurudi kundini mpaka umesafisha chama kile.”

Kauli hii ya Lembeli mbele ya Rais Magufuli pia Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)-Taifa baada ya kupewa nafasi ya kusema jambo kwenye mkutano huo, inaonekana kuwashangaza wengi.

Ikiwa ni siku moja tangu Lembeli ambaye alikuwa Mgombea Ubunge kupitia Chama cha Demokrasia (CHADEMA) kutoa kauli hiyo hatimaye Dk. Makongoro Mahanga amejitokeza na kumpinga.

Dk. Mahanga, aliyekuwa Naibu Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne na baadaye kujiunga na Chadema kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka jana amesema, hakutarajia Lembeli kutoa kauli tata ya kumshabikia Rais Magufuli.

“Rafiki yangu wa siku nyingi Lembeli, kaninyong’onyesha sana, hivi hajui kuwa mazuri yoyote ambayo Magufuli anayafanya, yanafutwa kabisa na utawala wa kidikteta pamoja na uminyaji wa demokrasia?”

Dk. Mahanga amesema, inasikitisha kuona Lembeli akisifia kazi za Rais Magufuli wakati anajua wazi kuwa, miongoni mwa kazi hizo kwa sasa ni pamoja na uminyaji wa demokrasia na vitendo vya kidikteta.

“Lembeli anaposifu kuwa, yanayofanywa na Rais Magufuli hata yeye alikuwa anayapigania miaka 10 iliyopita, ina maana Lembeli alikuwa anapigania nchi hii iendeshwe kibabe, kidikteta na kwa kufinyanga demokrasia?,” amehoji Dk. Mahanga.

error: Content is protected !!