ALIYEKUWA Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Joseph Magufuli (61), hadi mauti yanamfika saa 12:00 jioni ya Jumatano tarehe 17 Machi 2021, ameacha watoto saba. Anaripoti Regina Mkonde, Dodoma … (endelea).
Dk. Magufuli, alifikwa na mauti, akiwa Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo.
Soma zaidi:-
Leo Jumatatu, tarehe 22 Machi 2021, mwili wa Dk. Magufuli umeagwa kitaifa katika Uwanja wa Jamhuri, mkoani Dodoma ambapo wageni wa ndani na nje wameshiriki, wakiongozwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi, akisoma wasifu wa Dk. Magufuli amesema, alizaliwa Alhamisi ya tarehe 29 Oktoba mwaka 1959 “hadi mauti yanamfika, alikuwa na miaka 61.”
Amesema, Dk. Magufuli alikuwa mtoto wa tatu kati ya 12 ambapo “siku anazaliwa, bibi yake alikuwa amepika Pombe na hivyo akampa jina la walwa kwa kisukuma ikiwa na maana ya Pombe.”
Profesa Kabudi amesema, tatizo lililosababisha kifo chake la mfumo wa umeme, amekuwa nalo kwa zaidi ya miaka kumi.
Amesema, Dk. Magufuli, alifunga ndoa takatifu Kanisa Katoliki na Janeth mwaka 1989 ambapo “mpaka mauti yanamfika, ameacha watoto saba na waijukuu kumi.
Profesa Kabudi, amewataja watoto hao kuwa ni; Suzana, Edna, Mbalu, Joseph, Jesca, Yuden na Jeremia.
Mwili wa Dk. Magufuli, utazikwa nyumbani kwao, Chato mkoani Geita, Ijumaa ya tarehe 26 Machi 2021, siku ambayo imetangazwa kuwa ya mapumziko.
Marais waliohudhuria shughuli hii ni; Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Afrika (EAC), Filipe Nyusi wa Msumbiji, ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Felix Tshisekedi wa Congo, ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).
Wengine ni; Lazarus Chakwera (Malawi), Azali Assoumani (Comoro), Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, Edgar Lungu (Zambia), Mokgweetsi Masisi (Botswana) na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.
Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali
Leave a comment