October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Lwaitama: Tunapita kipindi kigumu

Spread the love

MWANAZUONI Dk. Azaveli Lwaitama amesema, Taifa linapita katika kipindi kigumu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, kutokana na wananchi wengi kukata tamaa ya kushiriki kwenye uchaguzi huo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Dk. Lwaitama ambaye ni Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ametoa kauli hiyo leo Jumamosi tarehe 13 Juni 2020, wakati akihutubia mkutano ulioandaliwa na Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo aliokutana na wadau wa jimbo hilo.

Dk. Lwaitama amesema, wananchi wengi watagoma kushiriki katika uchaguzi huo, kwa hofu ya kwamba wagombea wa Chama tawala CCM, watapita bila kupingwa.

“Kipindi hiki tunapita kipindi kigumu sana. Hapa nazungumza kama mwanazuoni, kuna hatari mbele ya safari, kuna watu watajichuja wakifikiri mgombea wa CCM atapita tu bila kuchaguliwa hilo ni kusaliti uraia wako,” amesema Dk. Lwaitama.

“Haiwezekani unafikiri jimbo la ubungo tunamhitaji fulani ukarudi nyuma kisa mgombea wa chama fulani atapita. Kwa nini unakubali mambo ya ajabu,” amesema.

Dk. Lwaitama amesema nchi inapita katika kipindi kigumu kutokana na baadhi ya watu wenye hulka ya kujipendekeza, kufanya mambo ya ajabu bila kutumwa, ili wapate vyeo.

“Tutapita kipindi kigumu, kipindi hiki kuna watu wanapenda kujipendekeza watafanya vitu ambavyo hawajatumwa na mtu yeoyote, sijui ili wateuliwe?” Amehoji  Dk. Lwaitama.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online & MwanaHALISI TV kwa habari zaidi

error: Content is protected !!