ALIYEKUWA Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, amesema bora amestaafu kuongoza Tanzania katika kipindi ambacho idadi ya watu ilikuwa ndogo, akisema kuongoza taifa lenye idadi kubwa ya watu ni kazi ngumu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Dk. Kikwete ametoa kauli hiyo leo tarehe 17 Novemba 2023, jijini Dar es Salaam, akizungumzia ongezeko la idadi ya watu nchini, katika hafla iliyoandaliwa kwa ajili ya kuzungumzia watoto wanaozaliwa kabla ya muda (njiti).
Amesema wakati alipokuwa madarakani alikuwa anaongoza watu milioni 42 na kwamba kutokana na ongezeko la idadi ya watu, miaka michache ijayo idadi hiyo itafikia milioni 70.
Mwanasiasa huyo amesema kuwa, idadi ya watoto wanaozaliwa kila mwaka ni 2,000,000 ambapo kati yao 300,000 ni njiti.
“…nashukuru nimestaafu maana ninapofikiria kuanza kuhangaika na watu milioni 70, hao milioni 42 walikuwa wananitoa jasho. Ninachotaka kusema tunaongezeka 2,000,000 kila mwaka na kati ya hao watoto njiti ni 300,000,” amesema Dk. Kikwete.
Dk. Kikwete amesisitiza mpango wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kusogeza karibu huduma za afya kwa wananchi, utekelezwe haraka ili kuokoa maisha ya wananchi hasa kina mama wajawazito na watoto wadogo.
Leave a comment