April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Kikwete amuomba Rais Magufuli kuichangia Yanga

Spread the love

DAKTARI Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne amemuomba Rais John Magufuli kuichangia Klabu ya Yanga. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Akizungumza kwenye harambee kubwa ya kuichangia Klabu ya Yanga, iliyofanyika leo tarehe 15 Juni 2019  katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam, Dk. Kikwete amesema hata yeye enzi za uongozi wake aliichangia Klabu ya Simba licha ya kwamba hakuwa shabiki wa timu hiyo.

Dk. Kikwete amemuomba Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu kumfikishia ujumbe huo Rais Magufuli, akisema kwamba hata yeye aliwahi kuisadia klabu ya Simba kiasi cha Sh. 30 milioni wakati akiwa rais, licha ya kwamba hakuwa shabiki wa timu hiyo.

“Nilipokuwa rais, Simba wanataka kununua kiwanja Mabwepande hela hawana, Aden Rage aliyekuwa rais wa Simba akaja kwangu akisema tumepata eneo kule tunatakiwa milioni 30 hatuna unatusaidiaje, nikawaambia mmepata, kwa hiyo pesa ikatoka sasa nasikia wanataka kujenga uwanja,” amesema Dk. Kikwete na kuongeza.

“Nasema haya kukumbushia ni wajibu wa uongozi, kwa hiyo waziri mkuu leo umekuja hapa Yanga wanachangisha toa, na umfikishie ujumbe mheshimiwa rais naye atoe. Na mie nilichangia milioni 30 Simba wakapata uwanja Mabwepande sasa mnatamba. Sisemi ni deni na nyie mlipe, ila nawaombea Yanga mchango kutoka kwako na rais.”

Dk. Kikwete amewakumbusha viongozi kwamba wakiwa kwenye uongozi wa serikali kila timu ya mpira ina wahusu, na kuwataka kutoshiriki katika vitendo vya ushabiki wa mpira kwa kugandamiza timu ambazo hawazishabikii.

“Sisi wote tuko kwenye taifa moja, na mkiwa kwenye uongozi wa serikali kila timu inakuhusu. Utakua kiongozi mwenye akili mbaya ukiwa kwenye uongozi, una dhamana unatumia ushabiki wako wa mpira kukandamiza timu nyingine, kwa sababu hata wasio timu yako kiongozi wake ni wewe,” amesema Dk. Kikwete.

error: Content is protected !!