November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Kijazi: Viongozi tengenezeni mazingira ya wananchi kuibua vivutio vya Utalii

Spread the love

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dk. Allan Kijazi ameutaka uongozi wa mkoa wa Lindi, wilaya Kilwa na vijiji vyake, kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya utalii kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA) ili kuwafanya wananchi kuibua na kuendeleza vivutio vya utalii vilivyopo na kuzitumia fursa hizo zilizoanzishwa. Anaripoti Christina Haule, Lindi … (endelea).

Dk, Kijazi alisema hayo jana wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa miundombinu hiyo uliofanyika kwenye magofu hayo yaliyopo Kilwa-Kisiwani mkoani Lindi.

Alisema ni mwaka mmoja umepita tangu TAWA ilipoanza kusimamia eneo hilo ambapo watalii wameongezeka kutoka 1200 mwaka 2018 hadi kufikia 2,340 mwaka 2020 na kufanya mapato kuongezeka kutoka Sh. 12 milioni hadi kufikia Sh. 40 milioni kutokana na TAWA kutangaza maeneo hayo ya utalii kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Akizungumza wakati akizindua miundombinu hiyo, Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi aliipongeza serikali kupitia TAWA kwa kuelekeza nguvu ya kuboresha miundombinu hiyo hatua ambayo itakuza utalii upande wa kusini mwa Tanzania.

Aidha Zambi aliishauri (TAWA) kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ili kurekebisha miundombinu ya wananchi wa jirani na eneo la utalii la Kilwa ikiwemo shule, kuweka maji na kuboresha zahanati kwa ajili ya huduma za matibabu.

“Mtu unakaa sehemu umezungukwa na maji halafu wewe huna maji hata ya kunywa, nadhani hilo haliwezekani, TAWA mnapaswa kuangalia hili, isiwe utalii kwa faida ya wengine bali kwanza waliopo waone faida zake,” alisema Zambi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA, Meja Jenerali Mstaafu Hamisi Semfuko amesema  mwaka 2018/19 Wizara ya Maliasili na Utalii ilifanya uamuzi wa kugawa mamlaka ya usimamizi wa vivutio vya malikale kwa taasisi za TAWA, TANAPA, TFS na NCAA na kuikabidhi TAWA kusimamia malikale za kunduchi, kilwa kisiwani na Songo/Mnara.

Meja Jenerali mstaafu Semfuko alisema kukamilia vizuri kwa eneo hilo kutafanya kuzidi kuwa kivutio muhimu kitakachovutia wageni zaidi na kuliingizia Taifa fedha za kigeni ili kufikia malengo yanayokusudiwa.

Aidha alisema katika kusimamia maeneo hayo TAWA ina wajibu wa kulinda kuhifadhi na kuendeleza magofu hayo na rasilimali nyingine zilizopo kwa kuzingatia sheria za kitaifa na kimataifa kwa faida ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

error: Content is protected !!