MUDA mfupi baada ya Paul Makonda, kuandika kwenye ukurasa wake wa Instagram, akimtaka mchekeshaji Idrisa Sultan ‘kujisalimisha’ katika kituo chochote cha polisi kwa madai ya kuvuka mipaka, Dk. Hamisi Kigwangalla ameibuka na kuahidi kumtetea. Anaripoti Martin Kamote … (endelea).
Makonda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, anamtuhumu Idriss kuvuka mipaka yake ya kazi, kwa kuchapisha picha ya Rais John Magufuli iliyohaririwa kisha na kuambatanisha ujumbe unaosomeka “kwa siku moja tukabadilishana kazi ili a-enjoy birthday yake kwa amani.”
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Dk. Kigwangalla amesema, iwapo Idriss atakamatwa na polisi kuhusiana na tuhuma hizo, atampatia mwanasheria wa kumtetea pamoja na kumuwekea dhamana.
“Nimeambiwa kuna msanii wa vichekesho anatafutwa na polisi, akikamatwa mniambie, nitajitolea mwanasheria wa kwenda kumuwekea dhamana na kumtetea. Rais wetu ni mtu wa watu na imejidhihirisha kwa jinsi wananchi walivyojitolea kumuombea dua siku ya kuzaliwa kwake! Wameonesha upendo,” ameandika Dk. Kigwangalla.
Nimeambiwa kuna msanii wa vichekesho anatafutwa na polisi, akikamatwa mniambie, nitajitolea mwanasheria wa kwenda kumuwekea dhamana na kumtetea. Rais wetu ni mtu wa watu na imejidhihirisha kwa jinsi wananchi walivyojitolea kumuombea dua siku ya kuzaliwa kwake! Wameonesha upendo
— Dr. Hamisi Kigwangalla (@HKigwangalla) October 30, 2019
Andiko la Dk. Kigwangala, Waziri wa Maliasili na Utalii linapuuza kile alichoandika Makonda “naona mipaka ya kazi yako huijui. Nenda sasa hivi kituo chochote cha polisi uwambie Makonda kaniambia nije, utakuta ujumbe wako.”
Idrisa ameandika ujumbe huo siku moja baada ya Rais Magufuli kusheherekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa tarehe 29 Oktoba 1959.
Leave a comment