Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Dk. Kigwangalla aomba radhi ‘mimi ni binadamu dhaifu’
Habari za Siasa

Dk. Kigwangalla aomba radhi ‘mimi ni binadamu dhaifu’

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Dk. Hamisi Kigwangalla
Spread the love

MBUNGE wa Nzega Vijijini (CCM), Dk. Hamis Kigwangalla amewaomba radhi watumishi na wananchi aliowakosea enzi akiwa waziri wa Serikali ya Tanzania. Anaripoti Brightness Boaz, Dar es Salaam … (endelea).

Dk. Kigwangalla ambaye alikuwa waziri wa maliasili na utalii katika baraza la mwisho wa Rais John Magufuli, lililomaliza muda wake 5 Novemba 2020, amesema hakufanya hivyo kwa kukusudia ilikuwa katika uwajibikaji.

Katika baraza jipya lililoapishwa leo Jumatano tarehe 9 Desemba 2020 na Rais Magufuli Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Dk. Kigwangalla hakuwa miongoni mwao na ametumua fursa hiyo kuandika ujumbe wa shukrani na kuopmba radhi.

Ujumbe huo ambao ameuweka kwenye akaunti zake za kijamii huu hapa chini;

Assalaam alaykum. Awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai. Miaka mitano iliyopita haikuwa rahisi kwangu: ilikuwa miaka ya kupanda na kushuka, ya kusimama na kuanguka, ya kujaribu na kufanya, ya kukosea na kupatia.

Ni kipindi kilichojaa furaha na maumivu, uhai na umauti. Ni kipindi nilichonusa kifo na kufufuka.

Ni kipindi nilichoshangilia na nilicholia machozi. Ni kipindi nilichopata ulemavu wa milele na maumivu yasiyoisha wala kusahaulika.

Siwezi kumlalamikia Mungu kwa lolote lile zaidi namshukuru kwa kuwa hai na kwa nyakati zote nilizopitia, za kiza totoro na za mwangaza. Kipindi hiki nilipewa heshima ya kuwa msaidizi wa Rais kwa nafasi nyeti serikalini (Afya na Maliasili na Utalii).

Naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mhe. Rais, John Pombe Magufuli, kwa imani yake kubwa kwangu, kwa maelekezo na usimamizi wake, si tu alikuwa kiongozi wangu mkuu bali pia alikuwa Mwalimu na Baba.

Sintosahau huruma na upendo alionionesha nilipopata ajali na msiba wa mwanangu.

Rais alipokea machela yangu huku akilia machozi, alihakikisha usalama na matibabu yangu wakati wote.

Ninawashukuru pia Makamu wa Rais (Samia Suluhu Hassan) na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) kwa uongozi na usimamizi wao wa karibu.

Kipekee ninawashukuru sana watumishi wote wa sekta za Afya na Maliasili niliohudumu nao kipindi nikiwa serikalini.

Tumepata mafanikio makubwa sana kwa uwezo wao na kwa kujitoa kwao, mara zote walinipa ushirikiano wa dhati kama moja ya viongozi wakuu wa sekta hizo. Ninawashukuru sana wadau wote wa sekta nilizohudumu.

Mara zote nilipokutana nao niliwasikiliza kwa umakini na kushughulikia changamoto walizokuwa nazo. Kimsingi walikuwa dira ya kazi zangu.

Hata hivyo, mimi ni binadamu dhaifu, sijakamilika, naomba radhi kwa kila niliyemkwaza ama kumuumiza. Haijawahi kuwa lengo langu bali ni jitihada za kujaribu kufanya mambo yafanikiwe.

Kazi ya kufanya jambo liwe zuri na timilifu siyo rahisi. Mimi sina kinyongo na mtu, na naomba sana niliowakwaza wanisamehe.

Nimempongeza Dk. Damas Ndumbaro, Waziri wa Maliasili na Utalii na nakusudia kesho kwenda kumkabidhi rasmi ofisi.

Nawapongeza mawaziri wote na nawaahidi ushirikiano wangu wakati wote.

2 Comments

  • Sawa kigwangala lkn je, Kama ungechaguliwa tena like your fellows hivi ungekumbuka kuandika haya??
    Nilitamani ungeyaandika haya ulipomaliza muda wako kabla ya uteuzi, ila sawa hujachelewa kuomba radhi isipokuwa nadhani it’s only because hujachaguliwa tena japo utafikiriwa kwenye nafasi zijazo watakapotumbuliwa wenzako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!