May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Hoseah aibua sakata la Richmond

Dk. Edward Hoseah mgombea urais chama cha wanasheria Tanganyika (TLS)

Spread the love

 

DAKTARI Edward Hoseah amesema, kilichomng’oa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ni kusema ukweli juu ya sakata la mkataba kati ya Serikali na kampuni ya kuzalisha umeme ya Richmond. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Dk. Hoseah amefichua siri hiyo leo Jumanne, tarehe 6 Aprili 2021, mkoani Dar es Salaam, alipokuwa akijibu swali aliloulizwa katika mdahalo wa wagombea urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Uchaguzi huo, unafanyika tarehe 15 Aprili 2021.

Dk. Hoseah aliondolewa katika nafasi hiyo na aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli, tarehe 16 Desemba 2015, huku sababu ikitajwa hakuridhishwa na utendaji wa Takukuru.

Hayati Magufuli, alichukua uamuzi huo ikiwa ni takribani mwezi mmoja tangu alipoingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015, akichukua nafasi ya Jakaya Kikwete aliyekuwa amemaliza muda wake.

Dk. Hoseah aliongoza taasisi hiyo nyeti, akiwa mkurugenzi mkuu kwa miaka tisa mfululizo, kuanzia tarehe 26 Novemba 2006, baada ya kuteuliwa na Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete na kuondolewa 16 Desemba 2015 na Hayati Magufuli.

Hayati John Magufuli aliyekuwa Rais wa Tanzania

Mmoja wa washiriki wa mdahalo huo, Raphael Awino amesema, tarehe 17 Desemba 2015, alisoma moja ya gazeti kwamba, Rais Magufuli (sasa ni marehemu), alimfukuza kazi Dk. Hoseah kwa kutoendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano.

“Je, kama ulishindwa kuonyesha mafanikio kwa miaka tisa, sasa mwaka mmoja wa TLS utauweza ambao mawakili wanamategemeo makubwa kwako na umeahidi mengi sana,” ameuliza Awino

Akijibu swali hilo, Dk. Hoseah amesema, aliondolewa katika nafasi hiyo, kufuatia msimamo wake wa kupinga sakata hilo la Richmond kufikishwa mahakamani, kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha.

“Hoseah na Richmond ndiyo mapambano yenyewe, mimi nahusiana nini na Richmond? Sina ninachohusika kwenye Richmond na sikuwepo kwenye manunuzi wala tenda. Nilichokisema kuwa ushahidi huu hauwezi kwenda mahakamani, hilo ndiyo kosa langu,” amesema Dk. Hoseah.

Dk. Hoseah amesema “kwa ushahidi huu, hauwezi kushinda, na mimi ni mwanasheria najua ushahidi huu ungepeleka mahakamani ingekuwa lafuzi tupu, nilisema wazi na public (umma) kwa ushahidi huu siwezi kwenda mahakamani.”

Amesema kosa lake lilikuwa hilo, na kwamba yeye hakuondolewa kwa kashfa yoyote ile.

“Hilo ndio kosa langu ndugu yangu, what do, I have to do with that scandle zinazosemwa? Historia inaonyesha anayepambana na rushwa kwa dhati hawezi kudumu katika hiyo nafasi,” amesema Dk. Hoseah.

Mbali na hayo, Dk. Hoseah amesema, kiongozi yoyote anayepambana na rushwa hupambana na watu wenye ushawishi mkubwa, ambao wanaweza kukusingizia jambo lolote, kama ilivyotokea kwake.

“Unapopambana na rushwa unapambana na mamlaka, maana yake unapambana na wenye ushawishi, unapambana pia na watu wenye fedha, hawa watu wana uwezo na ushawishi kwenye vyombo vya habari, utasingiziwa tu,” amesema Dk. Hoseah.

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete

Hata hivyo, Dk. Hoseah amesema, kama angepata nafasi ya kujitetea angejisafisha dhidi ya tuhuma hizo, lakini sheria za nchi haziruhusu suala hilo.

“Lakini la mwisho sisi hatuna nafasi ya kujitetea, ungenipa nijieleze zile kesi ungeshangaa, lakini sababu tunatawaliwa na kifungu 37 cha Sheria ya Kupambana na Rushwa, siruhusiwi kuongea katika kesi inayonihusu mwenyewe.”

“Lakini pia, Sheria ya Usalama wa Taifa kifungu cha 5 hakiniruhusu kujadili haya mambo, ningekuwa na uwezo wa kujadili kama unavyotaka walahi ungeshangaa , lakini sheria zinanizuia,”amesema Dk. Hoseah.

Akimalizia kujibu swali hilo, Dk. Hoseah amesema aliondoka Takukuru bila kashfa yoyote, na kuwaomba wanachama wa TLS wamchague kuwa rais wao.

“Mimi sina scandle (kashfa) nimeacha kazi serikalini na nimelipwa stahiki zangu zote, ningekuwa mwizi nisingelipwa haki zangu, mwizi halipwi. Hii kupakaziwa ni kawaida, niruhusini wana TLS niwape uzoefu wangu hamtajuta,” amesema Dk. Hoseah.

Kashfa hiyo ya Richond, ilitikisa nchi katika kipindi cha awali cha Rais Kikwete mwaka 2008.

Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu

Hii ilitokana na tatizo kubwa la uhaba wa umeme na Serikali kulazimika kutafuta njia za dharura zakutatua tatizo hilo, zikiwamo zilizodaiwa kukiuka taratibu na sheria.

Baada ya kashfa hiyo kuchunguzwa na taarifa kutolewa bungeni, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa alilazimika kujiuzulu baada ya kutakiwa ajipime kutokana na mazingira ya kashfa hiyo.

Lowassa, alitangaza kujiuzulu bungeni tarehe 7 Februari 2008 na nafasi yake, ilichukuliwa na Mizengo Pinda.

Wengine waliong’oka madarakani ni mawaziri wa Nishati na Madini kwa vipindi tofauti, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha.

error: Content is protected !!