May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Gwajima: Askofu Gwajima ni shemeji yangu, akamatwe

Spread the love

 

DAKTARI Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania, ameagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kumkamata na kumhoji Askofu wa Kanisa na Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuhusu tuhuma anazozitoa dhidi ya serikali juu ya chanjo ya corona. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mara … (endelea).

Amesema, licha ya Askofu Gwajima ambaye ni Mbunge wa Kawe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Dar es Salaam, kuwa shemeji yake, lakini amechoshwa na vitendo vyake.

Waziri Gwajima ametoa agizo hilo leo Jumanne, tarehe 17 Agosti 2021 akiwa Kijiji cha Kyatunge Wilaya ya Butiama mkoani Mara.

Agizo hilo amelitoa kipindi ambacho Askofu Gwajima amekuwa akitumia siku za Jumapili kanisani kwake, Ubungo Dar es Salaam, kuzungumzia chanjo ya corona ambayo inaendelea kutolewa nchini akisema yeye, rafiki zake na familia anazoziongoza hawatochanjwa.

Waziri wa Afya, Dorothy Gwajima na mumewe wakiwa katika mazoezi

Askofu Gwajima aliwatuhumu viongozi wa serikali kuhongwa ili kuruhusu kuingizwa nchini kwa chanjo hiyo ambayo tarehe 28 Julai 2021, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliizindua na Ikulu ya Dar es Salaam kwa kuchanjwa yeye mwenyewe na kuwaomba Watanzania kujitokeza kuchanjwa. Chanjo hiyo ni hiari.

Askofu Gwajima amekuwa akipinga chanjo hiyo kwamba si salama.

Hata hivyo, Waziri Gwajima amesema, mbunge huyo wa Kawe amekuwa akitumia kanisa lake kupotosha wananchi na kuzuia sintofahamu serikalini na kwenye jamii. Mme wa waziri ni kaka yake na Askofu Gwajima.

Waziri Gwajima amesema, Askofu Gwajima ambaye ni shemeji yake kujifanya msemaji wa wananchi kutoa kauli na tuhuma mbalimbali ikiwamo kwake mwenyewe (waziri) pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan.

Askofu Josephat Gwajima

“Askofu Gwajima ni ndugu yangu, ni shemeji yangu kabisa lakini mimi kama waziri wa wananchi nimekula kiapo mbele ya Rais cha kutumiakia nchi yangu sio kumtumikia shemeji yangu na mimi ndiye msemaji wa masuala ya afya, sasa nimechoka kuvurugwa vurugwa naagiza akamatwe popote alipo ahojiwe juu ya haya madai anayotoa,” amesema Waziri Gwajima

Waziri huyo amewashangaa wananchi wanaomuamini “huyu shemeji yangu Askofu Gwajima, hivi si ni yeye alisema atamfufua Amina Chifupa je alimfufua, hivi si ni yeye alisema ubunge ni jambo dogo hawezi kuwa mbunge lakini hivi sasa ni mbunge. Hivi si ni yeye alikutwa na mrembo akasema ni mkono wa baunsa..inakuwaje mnamuamini bado.”

Waziri Gwajima amesema, sekta ya afya sio ya kuchezewa na yeyote atakayejaribu kupotosha au kuvuruga mipango ya serikali lazima hatua kali zitachkuliwa bila kujali nafasi yake au uhusiano wake na mtu yeyote ndani au nje ya serikali.

error: Content is protected !!