April 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Gwajima abaini hasara bilioni 1 hospitali ya Tumbi

Spread the love

 

UCHUNGUZI wa tathmini ya uwepo wa thamani ya fedha katika utekelezaji wa mradi wa upanuzi na uboreshaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani-Tumbi umeonesha hasara ya Sh.1.6. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kibaha … (endelea).

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi tarehe 4 Machi 2021, na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima wakati akipokea tathmini ya awali ya mradi.

Dk, Gwajima, alitoa maagizo tarehe 24 Disemba,2020 alipotembelea hospitali hiyo, baada ya kutoridhishwa na ujenzi huo.

Katika ziara yake hiyo, Dk. Gwajima alitoa maelekezo kwa katibu tawala mkoa wa kufanya tathmini ya uwepo wa thamani ya fedha kwenye utekelezaji wa mradi wa upanuzi na uboreshaji wa hospitali hiyo na hasara imebainika kwa kuhakikiwa kwa baadhi ya vipimo vya kazi na kuchukua sampuli chache kwa ajili ya vipimo vya kimaabara jambo lililoashiria kuwepo kwa hasara kubwa zaidi kama ingefanyika tathmini ya kina.

“Ripoti nimeipokea na iko dhahiri kabisa mahitaji ya upanuzi na uboreshaji wa hospitali ya Tumbi yalikadiriwa kutekekezwa kwa Sh.29 bilioni baada ya Serikali kuonyesha nia ya kusaidia ufadhiri wa mradi huo kufuatia mpango wa awali wa uongozi wa Mkoa wa mwaka 2007-2009 iliokuwa na makadirio ya Sh.5,” amesema Dk. Gwajima.

Amesema mpaka sasa jumla ya Sh.9.4 bilioni zimekwishatolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kati ya Sh.29 bilioni, zilizokadiriwa ambapo Sh.5.5 bilioni, zimetumika katika utekelezaji chini ya usimamizi wa Shirika la Elimu Kibaha na Katibu Tawala Mkoa na Sh.3.9 bilioni zimehamishiwa wizara ya afya.

Hata hivyo, Dk. Gwajima amesema kupitia taarifa hiyo imebaini kuwepo kwa mikataba ya Wakandarasi wawili SUMA JKT na MUST Construction Bureau kinyume na Sheria namba 7 ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 pamoja na marekebisho yake mwaka 2016.

“Kutokana na mkanganyiko huo namuelekeza Katibu Tawala Mkoa kupitia Kamati yako ya tathimini, mfanye tathimini ya kina ndani ya siku thelathini na kuniainishia hasara halisi kwa kurejea vipimo vya jengo zima.”

“Kutathimini na kushauri kama jengo hili linafaa kwa matumizi ya Umma pamoja na Hali ya majengo ya zamani Kama yanafaa kukarabatiwa na kutumika Tena kwa gharama stahiki,” amesema Dk. Gwajima.

Licha ya hayo, waziri huyo, aliitaka kamati hiyo pia ihakiki uhalali wa uhitaji wa Sh.29 bilioni katika mpango wa upanuzi kwa kurejea michoro ya mpango, kuainisha sababu zilizopelekea wizara kurudia ununuzi wa mkandarasi wa awamu ya pili na ukidhi wa kisheria katika mchakato huo wa kumnunua mkandarasi mpya na kuagiza mradi huo usitishwe na madeni yasiendelee kulipwa mpaka atakapopokea tathimini ya kina na kuelekeza vinginevyo.

error: Content is protected !!