August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Dau apumua

Spread the love

KAULI ya Rais John Magufuli aliyoitoa jana wakati akifungua Daraja la Kigamboni kwamba, Watanzania wamekuwa wasahaulifu na kuwataka kuwa na kumbukumbu inaweza kumpa afueni Dk. Ramadhani Dau, anaandika Faki Sosi.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo ya kumpongeza Dk. Dau jana wakati wa ufunguzi wa Daraja la Kigamboni ambalo lilianza kutumia tarehe 16 Aprili mwaka huu.

‘Watanzania huwa tunasahau sana, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni’ alisema Rais Magufuli akimsifu Dk. Dau kutokana na kufanikisha ujenzi wa daraja hilo wakati akiwa Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo ikiwa ni wiki mbili baada ya kusambaa kwa taarifa kuwa, Dk. Dau, aliyekuwa mkurugenzi wa NSSF atafikisha mahakamani kutokana na matumizi mabaya ya ofisi na kulisababishia hasara shirika hilo.

Taarifa hizo zilisambaa baada ya zile za awali zilizoeleza kwamba, Dk. Dau alifikishwa na kuhojiwa na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), habari ambazo hazikuthibitishwa ama maofisa wa Takukuru au Dk. Dau mwenyewe.

Dk. Dau amekuwa midomoni mwa Watanzania wengi huku kila mmoja akiwa na mtazamo wake hasa baada ya kutenguliwa nafasi ya ukurugenzi aliyokuwa nayo ndani ya NSSF tarehe 15 Februari mwaka huu.

Kwenye ufunguzi wa daraja hilo Rais Magufuli amelimtaja Dk. Dau kuwa miongoni mwa watu muhimu waliofanikisha ujenzi wa daraja hilo ulioanza mwaka 2012 na kugharimu Dola za Marekani 128 milioni.

Daraja la Kigamboni lina urefu wa mita 680. Ujenzi wa daraja hilo ulifanywa na Kampuni ya China Railway 15 Group ikishirikiana na Kampuni ya China Bridge Engineering Group.

error: Content is protected !!