April 12, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Bisimba: Nchi imevimba

Dk. Helen Kijo Bisimba

Spread the love
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo-Bisimba, ameibuka na kusema, uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji wa juzi Jumapili, ulikuwa ni sawa na maigizo. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

“Sifahamu kama kulikuwa na uchaguzi. Sehemu kubwa ya wagombea walipita bila kupingwa. Na  maeneo machache, uchaguzi ulipofanyika, kulikuwa na dosari,” ameeleza.

Amesema, “kulikuwa na ukosefu wa vifaa katika maeneo karibu yote ya nchi. Haukuwa uchaguzi, ulikuwa ni maigizo; kwa sababu kulikuwa hakuna ushindani.” 

Dk. Bisimba ametoa kauli hiyo leo tarehe 26 Novemba 2019, katika mazungumzo yake na MwanaHALISI ONLINE kwa njia ya simu.

Amesema, uchaguzi huo ulikuwa maigizo kutokana na vyama vya upinzani kususia uchaguzi huo.

Hata hivyo, Dk. Bisimba amesema, mwitikio wa wananchi kupiga kura kwenye maeneo yaliyokuwa na uchaguzi ulikuwa mdogo, kwa kuwa wengi hawakuridhishwa na mazingira ya uchaguzi huo.

“Wengi hawakutaka kupiga kura kwa sababu wagombea wa vyama vyao wanavyotaka havikushiriki, kutokana na sababu mbalimbali, na kila mtu anapopiga kura huwa kuna kitu anakitaka. Lakini walichokitaka ambacho ilikuwa ni ushindani hawakupata,” amesema

Amekieleza Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa kisifikiri kiimeshinda uchaguzi, bali kimeshindwa. Amesema, maisha baada ya uchaguzi huo ni magumu.

Amesema, hali si nzuri kwa mustakabali wa taifa, kwani kuna uwezekano mkubwa kwa wananchi kutotoa ushirikiano kwa viongozi waliotangaza kuchaguliwa.

“Hali hii si nzuri, wana CCM wasifikiri wameshinda, wameshindwa. Na yale maisha baada ya uchaguzi ni magumu,  sababu kiongozi anatakiwa ashirikiane na wananchi. Kutokana na walio wengi kutochaguliwa na wananchi, wahusika wanaweza wakasusa kushirikiana nao. Kwenye ujenzi wa maendeleo ya maeneo yao husika pamoja na katika shughuli za kijamii,” ameeleza Dk. Bisimba.

Ameongeza: “uchaguzi huu umeonesha hatujengi nchi, tunaibomoa. Sababu kabla ya mfumo wa vyama vingi, nchi ilitaka kupinduliwa lakini baada ya mfumo wa vyama vingi, watu walijua tutapinduana katika vyama vyetu. Tukiendelea na hali hiyo, watanzania ni kondoo na kondoo ikifika wakati akichoka, anakuwa na hasira kali.”

Kwa mujibu wa Seleman Jafo, Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, CCM kimepata wenyeviti wa vijiji 12,260 kati ya 12,262, pamoja na mitaa yote 4,263 sawa na asilimia 100.

Amesema, kimepata wenyeviti wa vitongoji 63970 kati ya 63992, wajumbe kundi la wanawake 106,577 kati ya 106,622 na wenyeviti mchanganyiko 144,925 kati ya 145,021.

Kwa upande wa vyama vya upinzani ikiwemo vilivyojitoa kushiriki uchaguzi huo, Jafo alisema, Chadema haikufanikiwa kupata mtaa, lakini imepata mwenyekiti wa kijiji  mmoja, wa vitongoji 19, kundi la wanawake 39 na mchanganyiko 71.

Amesema, Chama cha Wananchi (CUF), kilipata mwenyekiti wa kijiji mmoja, vitongoji wawii, wajumbe kundi la wanawake watatu, huku mchanganyiko wakiambulia 14.

Huku ACT-Wazalendo,  kikipata mwenyekiti wa kitongoji mmoja, mjumbe mmoja kundi la wanawake na wajumbe 11 mchanganyiko.

vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo, UDP kimepata nafasi moja ya mjumbe katika kundi la wanawake na DP kimepata sawa na UDP.

error: Content is protected !!