July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Bilal kushuhudia mkesha Dar

Viongozi wa Kamati ya Mkesha wa Mwaka Mpya

Spread the love

MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal atakuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa mkesha wa Mwaka Mpya wa 2015 utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, anaandika Sarafina Lidwino.

Mwenyekiti wa Mkesha huo, Mchungaji Godfrey E. Malassy, amewaambia waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari Maelezo, kwamba wakazi wa jiji la Dar es Salaam watapatiwa huduma ya usafiri wa bure kwenda na kurudi uwanjani, kwa kutumia mabasi yaliyotolewa na Shirika la Usafiri la Dar es Salaam (UDA).

Mchungaji Malassy amesema UDA limetoa mabasi 200 kwa ajili hiyo kama mchango wao wa kurahisisha misafara ya wakazi wa jiji na vitongoji vyake watakaohudhuria mkesha huo ambao pia alisema utafanyika kwenye miji ya Mbeya, Iringa, Ruvuma, Mtwara, Bukoba na Zanzibar.

Ameishuruku menejimenti ya UDA kwa mchango wao huo muhimu uliolenga kufanikisha mkusanyiko wa kuombea amani taifa la Tanzania.

Mchungaji Malassy amesema viongozi wa dini na madhehebu yote wameamua kufanya mkesha huo mkubwa wa kitaifa mwisho wa mwaka kama ilivyo miaka yote kama hatua ya kuungana na Watanzania wote katika maombi ya amani kwa nchi inapoingia mwaka wa uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

“Watanzania tunajua amani inatoka kwa Mungu, na kwa sababu hiyo ndio maana hatuna vita kama nchi za jirani wanasema Tanzania ni kisiwa cha amani kutokana na utulivu tulionao na tunatunza amani yetu, na naomba tujitokeze kwa wingi kwenye mkesha ili tuombe kwa umoja wetu,” amesema.

“Wanasiasa wengine wanajaribu kuvunja amani kwa kutishia kuuwa au kumwaga damu za wananchi kwa visingizio mbalimbali, wengine hufanya hivyo kwa shauku ya kupata uongozi.   Wanaodhani amani hupatikana kwa mtutu wa bunduki wamelaaniwa,” amesema.

Amesema wananchi wajitokeze kwa wingi huku wakihakikishiwa ulinzi utakuwa imara kutokana na ahadi ya Jeshi la Polisi mkoani Dar es Salaam.

error: Content is protected !!