April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Bashiru, Zitto wachuana

Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM

Spread the love

ZITTO Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo na Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wapo ‘mtaani’ kukusanya maoni ya wananchi. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Ikiwa imebaki takribani miezi 10 kuingia kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ACT-Wazalendo na CCM vimeanza kukutana na wananchi na kusikiliza maoni yao ikiwa ni hatua za awali za kujiandaa na uchaguzi huo.

Tayari Zitto amepita kwenye maeneo mbalimbali yenye mikusanyika ya watu, ikiwemo sokoni na kwenye vijiwe jijini Dar es Salaam, kuzungumza na kukusanya maoni yao.

Ziara ya Zitto jijini Dar es Salaam ameipa jina la ‘listening tour,’ kwa maana ya ziara ya kusikiliza kero, maoni na dukuduku kutoka wa wananchi.

Miongoni mwa maeneo ambayo ametembelea ni pamoja na Jimbo la Segerea, Mbagala na Temeke. Kwenye ziara hiyo, Zitto aliongozana na maofisa waandamizi wa chama hicho.

“….hasa sisi kinamama tukienda Temeke kujifungua, mpaka uwe na shilingi 85,000 ndio upate huduma ya kujifungua, na kama umeandikiwa oparesheni lazima uwe na 180,000 ndio upate huduma hiyo. Asilimia 90 ya wanawake tunalalamika,” mama mmoja ambaye hakutaja jina lake alimueleza Zitto.

Wakati Zitto akiendelea kuzungumza na wananchi wa rika lote, Dk. Bashiru naye ameingia ‘mtaani’ kukusanya maoni ili kutengeneza Ilani ya CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kiongozi huyo wa CCM, ameagiza kamati za siasa za wilaya na mikoa kuanza kukusanya maoni ya wananchi na kisha kuwasilisha makao makuu ya chama hicho ili yachakatwe na kisha kuingiza kwenye Ilani.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika mwaka 2020, huku vyama vya siasa vikianza kuangazia uchaguzi huo.

Taarifa ya Dk. Bashiru imetolewa na Said Nguya, Ofisa Habari wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, na kwamba uamuzi huo ni sehemu ya maazimio ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.

error: Content is protected !!