May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Bashiru: Unafiki unakwamisha kufikia malengo

Spread the love

MBUNGE wa Kuteuliwa (CCM), Dk Bashiru Ally amesema, unafiki na kukosekana uzalendo kwa baadhi ya watu ni sababu ya mambo yanayokwamisha kufikia malengo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Amesema hayo juzi Jumatatu, tarehe 28 Juni 2021, bungeni jijini Dodoma, katika kikao cha kamati ya kilimo, uvuvi na maji na wadau wa uzalishaji wa mafuta ya alizeti kupitia mradi wao wa Policy Analysis Group (PAG).

Dk Bashiru aliwahi kuwa katibu mkuu wa CCM na Katibu Mkuu Kiongozi, nafasi aliyohudumu kwa muda mfupi kabla ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mbunge.

Alisema bado unafiki umewajaa baadhi ya wengi ingawa wanatamba kwa kauli ya tuko pamoja kitu alichosema haamini kama kweli wako pamoja kama wanavyotamka midomoni mwao.

Alisema Taifa haliwezi kufikia malengo yake ikiwa watu hawatabadili mitazamo yao na kusimamia ukweli kwa mambo yanayoleta maendeleo halisi ya wananchi na Taifa lao huku akikosoa mpango wa usimamizi wa ardhi.

“Tatizo la usimamizi wa ardhi ni donda ndugu, mfumo wake hauko vizuri, hasa tunapotaka wakulima wadogo wabebe uchumi kupitia kilimo, sidhani kauli za tuko pamoja kama kweli zina uhalisia wake, lazima tubadilike,” alisema Dk Bashiru, aliyewahi kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kuhusu upungufu wa mafuta ya kula, Dk. Bashiru alisema, kuna shida ya kupanga na akasisitiza mikakati ya kuondoa upungufu wa mafuta inatakiwa kwenda sambamba na mkakati wa kumaliza upungufu wa ngano na sukari ili navyo viwe kwenye mkakati.

Kwa mujibu wa Dk. Bashiru, kauli za kuwa ipo ardhi ya kutosha kwa kilimo alisema hazina ukweli wala kwani licha ya kuwepo lakini sehemu kubwa ardhi hiyo inamilikiwa na watu ambao wanafanya biashara ya kukodisha kwa wakulima hivyo kwa asiye na uwezo hawezi kulima shamba kubwa.

Naye Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage alikosoa mikakati ya kumaliza uhaba wa mafuta kwamba huenda isisaidie kitu kwa sababu imekuwa ya kutamkwa mdomoni lakini ukweli haupo hivyo.

Mwijage aliyewahi kuwa waziri wa viwanda na biashara, alisema katika uongozi wake akiwa Waziri aliweka mkakati wa kumaliza tatizo la mafuta ya kupikia nchini lakini hadi sasa mpango wake haujafanikiwa badala yake anaona wadau wanakuja na mpnago mwingine bila kueleza wa kwanza walishindwa wapi.

Mwijage alisema ni lazima Serikali iingize kwenye mipango yake ikiwemo kurudisha utarataibu hata wa kununua matrekta na kuwapa maeneo halisi ya kulima ili mtu mwenye shamba dogo awe na ekari walau 10.

Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Kilimo, Timoth Mbaga alisema soko la mafuta ni kubwa nchini kwani utoshelevu wa mafuta kwa sasa ni asilimia 45 na kiasi kinachobaki kinaagizwa nje lakini akasema mikakati mizuri waliyonayo inaweza kufikisha malengo na ziada ikauzwa nje.

Mbaga alisema, asilimia 95 ya wazalishaji na wakulima wa alizeti ni wakulima wadogo ambao wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mbegu bora na hamasa ya kilimo cha zao la alizeti.

error: Content is protected !!