NAPE Nnauye, Mbunge wa Mtama na Hussein Bashe, Mbunge wa Nzega Mjini ni miongoni mwa wanasiasa vijana wanaomvutia Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Akimzungumzia Nape katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha ZBC2 leo tarehe 26 Aprili 2019, Dk. Bashiru amesema, ni kiongozi mzuri na kwamba, kuna baadhi ya maeneo anahitaji kupikwa.
Nape ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Itikadi na Uenezi wa CCM pia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ametajwa na Dk. Bashiri kwamba ni jasiri.
Dk. Bashiri alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na mtangazaji maoni yake kuhusu misimamo ya wabunge wa CCM ambao wamenukuliwa wakitoa kauli kali kwa serikali iliyoko madarakani.
“Nape ni mwenezi wetu, jasiri kabisa lakini anahitaji kupikwa,” amesema Dk. Bashiri akiongeza “nilichokuwa nasema siyo nakubali kila kitu, bali mtambue kuwa, chama kina wajibu wa kuwasikiliza, kuwaandaa, kuwaamini na kuwasimamia kama wanakwenda inavyotakiwa.”
Dk. Bashiru amesema, kutokana na mazingira ya sasa yalivyo, Nape na Bashe ni kati ya watu ambao wana mchango mkubwa.
Amesema, kutokana na umuhimu wa kuandaa vijana, wameomba kijengwe chuo cha kuandaa viongozi kutoka nchi sita tofauti.
“Lengo ni kuandaa viongozi waliochipukia kwa sababu suala hili linahitaji maarifa na bila shaka tutakuwa na kina Nape na Bashe wengi,” amesema Dk Bashiru.
Leave a comment