May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Bashiru alipa kibarua Bunge

Spread the love

 

MBUNGE wa kuteuliwa na Rais, Dk. Bashiru Ally, amelishauri Bunge la 12 lijikite katika ajenda za kuchochea mapinduzi ya kilimo, kama Bunge la 11 lilivyofanikiwa kuchangia mabadiliko katika sekta ya madini. Anaripoti Jemima Samwel,DMC…(endelea).

Dk. Bashiru alitoa ushauri huo jana tarehe 25 Mei 2021, akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, bungeni jijini Dodoma.

Mwanasiasa huyo alitoa ushauri huo baada ya wabunge wengi kulalamikia udumavu wa sekta ya kilimo, uliochangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa masoko ya mazao ya kilimo na uzalishaji mazao yasiyo na tija.

“Bunge la 11 katika historia litatambulika kwa kuleta mabadiliko makubwa sana, ya kisera na kisheria kwenye sekta ya madini na tumeona matokeo yake. Hili la 12 chini ya uongozi wako (Spika Job Ndugai), tujipe jukumu la kubadilisha sekta ya kilimo,”

“ Ili hizi sifa mbaya za tija duni, ukosefu wa masoko na kutoongeza thamani mazao ya kilimo, zibadilike. Ili tufanane na sekta nyingine zinazobadilika haraka, kama vile miundombunu, mawasiliano na kadhalika,” alisema Dk. Bashiru.

Aidha, Dk. Bashiru alilitaka bunge hilo, litafute majibu ya sababu za kasi ya maendeleo katika sekta nyingine haiendi sambamba na sekta ya kilimo.

“Swali la kuzingatia katika Bunge hili la 12, linaweza kutoa mchango gani mpya katika kuchochea mapinduzi ya kilimo,” alisema Dk. Bashiru.

Dk. Bashiru aliongeza “ swali la tatu, tuweze kujibu hoja kwa nini mabadiliko makubwa yaliyotokea katika sekta ya miundombinu, fedha, sayansi na teknolojia, ongezeko la watu, elimu na mawasiliano, havichochei ukuaji wa kilimo?”

Wakati huo huo, Dk. Bashiru alilitaka Bunge hilo, lijadili sababu za changamoto sugu katika sekta ya kilimo, kukosa ufumbuzi kwa muda mrefu.

“Nakuomba spika ama unaweza kuelekeza kamati yetu , au kwa busara yako kufikiria namna ya kufanya kujibu maswali swali hili, tunajifunza nini kutokana na mafanikio tuliyopata katika sekta ya kilimo, lakini na makosa tuliyofanya kwenye sekta ya kilimo,” alisema Dk. Bashiru.

error: Content is protected !!