April 11, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Abbas apinga uamuzi wa Rais Samia

Dk. Hassan Abbas, katibu mkuu wizara ya habari

Spread the love

 

KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbasi, amepinga maagizo ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ya kufungulia vyombo VYOTE vya habari vilivyofungiwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Jana Jumanne tarehe 6 Aprili 2021, Rais Samia alitoa amri ya kuacha huru vyombo vyote vya habari nchini akiwa Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akihutubia baada ya kuwaapisha makatibu, manaibu katibu wakuu na viongozi wa taasisi za umma.

Rais Samia alisema, wizara ya habari inapaswa kusimamia vyombo vya habari “nasikia kuna vijivyombo vya habari mmevifungia fungia, sijui viji- TV vya mikononi vile, vifungulieni lakini wafuate sheria na miongozo ya serikali.”

“Vifungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunabinya uhuru wa vyombo vya habari, lakini mhakikishe kila mliyempa ruhusu ya kuendesha chombo cha serikali anafuata sheria za serikali na kanuni ziwe wazi, kosa hili adhabu yake ni hii na mnakwenda kwa adhabu mlizoziweka kwenye kanuni,” alisema

Katika kusisitiza hilo, Rais Samia alisema “tusifungie tu kibabe. Wafungulieni lakini tuhakikishe wanafuata kanuni na miongozo ya serikali.”

Baadhi ya vyombo vya habari vilivyofungiwa, futiwa leseni au kunyimwa leseni za uendeshaji ni MwanaHALISI, Mawio, Tanzania Daima, Mseto na televisheni ya mtandaoni ya Kwanza TV.

Kauli hiyo ya Rais Samia imepongezwa na wadau mbalimbali wa habari ikiwemo Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), lililosema, hatua hiyo ni mwanzo mzuri na kumuahidi ushirikiano utakaozingatia weledi wa kazi hiyo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Dk. Hassan Abbas ambaye wakati magazeti yanafungiwa au kunyimwa leseni alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, alizungumzia maagizo hayo ya Rais Samia.

Akizungumza na moja ya chombo cha habari, Ikulu ya Dar es Salaam, mara baada ya kumaliza hafla ya uapisho, Dk. Abbas alisema, maagizo hayo yanahusu televisheni za mtandaoni na si magazeti.

Dk. Abbas ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari aliyewahi kufanya kazi kwenye magazeti, ikiwemo Gazeti la Majira, alidai agizo hilo lilikuwa maalumu kwa vyombo hivyo, kwa kuwa kiongozi huyo wa nchi amefanya marekebisho katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ambayo ni msimamizi wa vyombo hivyo.

“Unajua kwanza hilo ni agizo la Amiri Jeshi Mkuu, ni rais lakini pia uzingatie ndio kiongozi wetu, na alikuwa specify (taja) kabisa kuna online tv ambazo zimefungiwa na unafahamu pia amefanya mageuzi kule TCRA.”

“Kwa hiyo kwanza leo (jana) tunakwenda kuona ni online tv gani ambazo zimefungiwa, kwa sababu gani na kuchukua hatua kama alivyoelekeza. Lakini alisisitiza vyombo viendelee kuzingatia maadili sheria za nchi,” alisema Dk. Abbas

Alisema agizo hilo limeanza kufanyiwa kazi na hivi karibuni atatoa orodha ya vyombo vya habari vya mtandaoni vitakavyofunguliwa.

“Lakini kwa hivyo alivyoagiza tunatenda kuchukua hatua mara moja, tutaiona hiyo orodha ni ipi na tutatoa kwa umma watu wajue Tv gani zimeachiwa,” alisema

Alipoulizwa kuhusu magazeti yaliyofungiwa, Dk. Abbasi alisema, kama watapata maelekezo mengine juu ya suala hilo watalifanyia kazi, lakini kwa sasa wanashughulikia vyombo vya habari vya mitandaoni pekee.

“Kama nilivyosema, leo (jana) ame-specify kwenye online tv, tutalifanyia kazi hilo lakini kama kuna maelekezo mengine, pia tutachukua hatua kama good will ambayo anaitoa. Watu waendelee kufanya kazi lakini wazingatie sheria pia,” alisema Dk. Abbasi

Hata hivyo, taarifa kwa umma, iliyotolewa jana Jumanne na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa ilizungumzia masuala mbalimbali yaliyojili kwenye hafla hiyo.

Msigwa ambaye pia kwa sasa ndiye Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, alisema Rais Samia ameagiza “vyombo vya habari vilivyofungiwa vifunguliwe na kutakiwa kuzingatia sheria.”

Kauli hiyo ya Dk. Abbas ambayo inaashiria kupinga maagizo ya bosi wake, Rais Samia ambaye yeye alieleza vyombo vyote vilivyofungiwa kufunguliwa, imepokewa kwa hisia tofauti na watu mbalimbali na kuzia mjadala mitandaoni.

Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena, katika ukurasa wake wa Twitter ameandika, “katibu mkuu wizara ya habari, Dk. Hassan Abbas bado ana ‘hamu’ ya kuendelea kufungia magazeti kwa kutafsiri maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan eti amri yake inahusu kufunguliwa kwa Online TV t. Ndugu yetu huyu hajifunzi.”

Aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk. Ananilea Nkya naye ameandika Twitter “Dkt Abbas, Rais Tanzania SSH amesema vyombo vya habari viivyofungiwa vifunguliwe.”

“Wewe umeibuka na kusema ni vyombo fulani tu. Mbona unakwenda kinyume na maagizo ya Rais? Wewe kitaaluma ni mwanahabari kwa nini umeamua kuwa adui wa vyombo vya habari.?”

error: Content is protected !!