DIWANI wa kata ya Ubungo anayemaliza muda wake kwa tiketi ya Chadema, Boniface Jacob leo amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu, akituhumiwa kumpiga na kumjeruhi mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru, Christopher Lisso. Anaandika Mwandishi Wetu … (endelea).
Mbele ya hakimu Hellen Liwa, wakili wa serikali Kenneth Setwao amesema Boniface Jacob anatuhumiwa kutenda kosa hilo Septemba 11, 2015 katika Wilaya ya Kinondoni.
Mtuhumiwa amesomewa mashtaka mawili, kosa la kwanza Setwao amesema mtuhumiwa alimpiga mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru, Christopher Lisso na kumsababishia maumivu sehemu mbalimbali za mwili wake.
Wakili huyo wa serikali Amesema katika shitaka la pili mtuhumiwa anatuhumiwa kuharibu kamera yenye thamani ya Sh 8 milioni, mali ya kampuni ya Uhuru Publications Limited.
Mtuhumiwa anayetetewa na wakili wa kujitegemea, John Mallya amekana mashtaka yote mawili na yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza matakwa yaliyowekwa ya kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini dhamana yenye thamani ya Sh 8 milioni.
More Stories
ACT-Wazalendo yasema bei ya vyakula imepaa, yatoa mapendekezo
CCM yataka viingilio Sabasaba vipunguzwe
Mahakama yasema uamuzi kesi ya kina Mdee haujakamilika