Tuesday , 23 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Diwani wa CCM avunja rekodi
Habari za Siasa

Diwani wa CCM avunja rekodi

Spread the love

 

DIWANI wa Kata ya Mzimu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Manfred Lyoto amepongezwa kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wake ndani ya muda mfupi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Pongezi hizo zimetolewa jana Jumapili, tarehe 8 Januari 2023 na baadhi ya wananchi wa viongozi wa Kamati ya Siasa ya CCM Kata ya Mzimu, wakati Lyoto anawasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho, katika kipindi cha miezi sita iliyopita (Juni hadi Desemba, 2022).

Akielezea utekelezaji wa ilani hiyo, Diwani Lyoto alieleza miradi iliyotekelezwa katika kata hiyo kwenye sekta ya afya, elimu, miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Kwenye sekta ya afya, Diwani Lyoto alisema kwa kutumia gharama zake aliwakatia bima za afya wazee 20, zenye thamani ya Sh. 800,000. Kukamilisha ujenzi wa choo cha Zahanati ya Mzimuni kwa kununua vifaa vya ujenzi vyenye thamani ta Sh. 1.4 milioni. Kuwalipa posho kila mwezi kiasi cha Sh. 1,000,000 watumishi watatu wa afya wanaojitolea katika zahanati hiyo.

“Katika zahanati yetu kulikuwa na daktari mmoja na nesi mmoja, wananchi wanaokwenda wanakuwa wanasubiri masaa mengi kutibiwa nikaona tutawauwa watu. Nimeajiri daktari mmoja, nesi mmoja na mtu mmoja wa maabara,” alisema Diwani Lyoto.

Katika hatua nyingine, alisema mfadhili amepatikana kwa ajili ya kujenga wodi ya kina mama kujifungua watoto.

Kuhusu sekta ya elimu, Diwani Lyoto alisema amewaajiri walimu wa masomo ya sayansi watano katika Shule ya Sekondari Mzimuni, ambapo kila mmoja anamlipa Sh. 500,000 kila mwezi, kununua mashine ya uchapishaji iliyogharimu Sh. 3 milioni, pamoja na kusimamia ujenzi wa ukuta unaozunguka shule za kata hiyo, Shule ya Sekondari Mzimuni, Shule ya Msingi Mikumi na Mzimuni, uliogharimu Sh. 70 milioni.

“Aprili 2022 tulianza rasmi maandalizi ya mpango wa lishe shuleni kwa kutengeneza miundombinu ya jiko kwa gharama ya Sh. 1.5 milioni. Kununua vifaa vya kupikia kwa gharama ya Sh. 2 milioni, ununuzi wa kontena kwa ajili ya matumizi ya stoo ya vyakula lililogharimu Sh. 7.5 milioni. Gharama zote ni kutoka mfuko wangu binafsi,” alisema Diwani Lyoto.

Kwa upande wa sekta ya ajira, Diwani Lyoto alisema ofisi yake ilisaidia vijana wa Kata ya Mzimuni takribani 70 kupata ajira, ikiwemo za udereva, viwandani na biashara.Pia, amesema katika jitihada za kuwainua kiuchumi wananchi wake, alisimamia upatikanaji wa mikopo ya halmashauri Sh. 154 milioni, pamoja na kuanzisha Lyoto Foundation, ambayo itatoa mikopo kwa wananchi bila masharti na riba.

Awali, Mwenyekiti wa msafara wa kukagua miradi iliyotekelezwa na Diwani Lyoto kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Fadhil Konja, alisema “tumefarijika na utekelezaji wa ilani ya CCM unao tatua shida za wananchi ikiwemo ujenzi wa mifereji katika barabara za mitaa minne ambao umesaidia kupunguza mafuriko.”

Naye Mkuu wa Shule ya Secondari Mzimuni, Juma Righton, amemshukuru Diwani Lyoto kwa kuwajengea ukuta uliogharimu Sh. 70 milioni, ambao umeisaidia wanafunzi shule hiyo na shule jirani (Shule ya Msingi Mikumi na Mzimuni), kusoma kwa utulivu pamoja na kudhibiti vitendo vya utoro.

Mwalimu Righton alimshukuru Diwani Lyoto kwa kuwaajiri walimu watano wa masomo ya sayansi katika shule yake.

Aidha, Mwalimu Righton amemshukuru Diwani Lyoto kwa kununua mashine ya kutoa nakala iliyogharimu kiasi cha Sh. 3 milioni, kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo uchapishaji mitihani kwa shule hizo tatu.

Kwa upande wake mkazi wa kata hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Mama Kipengule, amemshukuru Diwani Lyoto kwa kusimamia ujenzi wa barabara za mitaa sambamba na kuweka mifereji, kitendo kilichowasaidia kuepukana na adha ya mafuriko.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

Habari za Siasa

Rais Samia aridhishwa utendaji mabalozi, awapa neno

Spread the loveRais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amewapongeza mabalozi  wanaowakilisha ...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NMB yadhamini Mkutano Mkuu ALAT, kufunguliwa na Samia

Spread the loveBENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. 120...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

error: Content is protected !!