June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Diwani CUF aahidi kumng’oa Mkurugenzi Dodoma

Spread the love

MGOMBEA udiwani kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) Damasi Thadei, Kata ya Ipagala manispaa ya Dodoma amesema iwapo wananchi watampa ridhaa ya kuwa diwani wa kata hiyo jambo la kwanza ni kupambana na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Diwani huyo amesema kama Mkurugenzi wa Halmsahauri hiyo akishindwa zinapatikana asilimia kumi ya mapato ya halmashauri kwa ajili ya maendeleo ya akina mama na vijana, hawezi kubaki.

Mbali na hilo amesema jambo lingine ni kuhakikisha vijana wa kata hiyo wanapatiwa ardhi na kupatiwa hati za kumiliki ardhi hiyo ili waweze kutumia ardhi yao kwa kujiendelea na kuwapatia uhalali wa kukopa katika mabenki mbalimbali.

Mgombea huyo alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya soko jipya la Mbuyuni ambalo lipo Ilazo West mjini hapa.

Thadei amesema tangu kuwepo kwa kata hiyo ambayo imekuwa ikiongozwa na madiwani wa CCM kwa nyakati tofauti wameshindwa kutatua tatizo la migogoro ya ardhi.

“Kila mtu anajua katika kata hii ya Ipagala kuna migogoro mikubwa ya ardhi hapa kuna Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) imekuwa ikishirikiana na viongozi mbalimbali wakiwepo madiwani waliomaliza muda wao kwa kujigawia viwanja huku wananchi wakiendelea kunyanyasika kwa kukosa viwanja vyao.

“Mbaya zaidi ni pale ambapo watu ambao ni wazawa waliokuwa wakimiliki mashamba yao tangu zamani lakini wamekuwa wakiporwa mashamba yao na kupimwa na kuuzwa kwa wageni huku wenyeji wakikosa viwanja ama kuuziwa kwa bei kubwa,” amesema Thadei.

Amesema ni lazima vijana wakaandaliwa mpango wa kumilikishwa viwanja na kupatiwa hati miliki ili kuwawezesha kutumia hati hizo kukopa katika taasisi za kifedha ili waweze kufanyabiashara mbalimbali hata kwa kununua boda boda kama sehemu ya kujiajiri.

Kuhusu kuwawezesha vijana Thadei amesema iwapo atapata nafasi ya kuwa diwani wa kata hiyo atahakikisha uongozi wa kata kwa kushirikisha halmashauri vijana wote wanaojuhusisha na Bodaboda wanatengewa maeneo ambayo yatakuwa rafiki katika kufanya kazi zao sambamba na akina mama lishe.

Katika mkutano huo alisema haiwezekani serikali ya CCM kuendelea kuwabeza akina mama wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wazee kuwa wanatibiwa bure wakati wanaendelea kununua dawa licha ya kuwa familia nyingine zimejiunga katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kuchangia fedha zao kwa uaminifu.

Kutokana na hali hiyo alisema umefika wakati wa UKAWA kuchukua nchi ili kurekebisha mifumo mibovu ya chama cha Mapinduzi ambayo ni yaukandamizaji, unyonyaji na wizi wa rasilimali za Umma.

Thadei amesema kutokana na kuwepo kwa muunganiko wa vyama vinne vya siasa ambavyo vinaunda UKAWA ni wakati sasa wa kuwapigia kura nyingi viongozi wanaotokana na UKAWA.

error: Content is protected !!