Friday , 29 September 2023
Home Habari Mchanganyiko Dilunga aagwa: CCM, Chadema ACT-Wazalendo watoa ujumbe 
Habari Mchanganyiko

Dilunga aagwa: CCM, Chadema ACT-Wazalendo watoa ujumbe 

Mwili wa Godfrey Dilunga ukiagwa
Spread the love

KIFO cha Godfrey Dilunga, aliyekuwa Mhariri wa Gazeti la Jamhuri kilichotokea alfajiri ya tarehe 17 Septemba 2019, kimeunganisha wanasiasa wa upinzani na chama tawala. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Wakizungumza katika nyakati tofauti kwenye shughuli ya kuuaga mwili wa Dilunga iliyofanyika leo tarehe 19 Septemba 2019 kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, wanasiasa hao wamesema watamkumbuka kutokana na hulka yake ya kuheshimu tofauti za kila mtu hasa za kiitikadi na kisiasa.

Humphrey Polepole, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM amesema kitu ambacho atajifunza kutoka kwa marehemu Dilunga ni ustahimilivu wake katika tofauti za hoja na kujifunza.

Pia, Polepole amesema CCM itamkumbuka Dilunga kwa mchango wake ndani ya chama hicho pamoja na kuitumia vyema kalamu yake pasipo kumuonea na au kumpendelea mtu kwenye uandishi, enzi za uhai wake.

“Ambacho najifunza kutoka kwa Dilunga ilikuwa ni kuhusu ustahimilivu na kujifunza. Pia, hakutumia kalamu yake kumsema mtu kile ambacho hakikustahili,” amesema Polepole.

Maneno ya Polepole hayakuachana mbali na maneno ya Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo aliyesema kwamba Dilunga alikuwa anaheshimu maoni, msimamo na hoja ya kila mtu, na hasa ya mtu ambaye alikuwa mpinzani wake.

Zitto amesema Dilunga enzi za uhai wake, alikuwa mhariri mwenye kusimamia maadili, aliyefanya kazi zake kwa ukweli, uwazi pasina upendeleo.

“Leo hii Dilunga anaheshimiwa na kila mtu kwasababu ilikuwa ukiwa mpinzani wake anakuheshimu zaidi. Alikuwa ni mtu anayeheshimu mawazo tofauti na hata akiwa hakubaliani na wewe hakutukani,” amesema Zitto na kuongeza;

“Enzi za uhai wake, Dilunga akikuchapa katika tahariri lazima umtafute. Lakini alikuwa anasimamia ukweli. Ni miongoni mwa wahariri wachache wenye tabia hiyo. Jukwaa la Wahariri wanapaswa kuwa na kazi ya ziada kutengeneza wahariri wa aina ya Dilunga.”

Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Chadema Zanzibar, amesema enzi za uhai wake, Dilunga alifanya kazi na vyama vyote pasina na upendeleo, huku akikumbushia mchango wake katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambapo alifanya kazi na vyama vyote.

Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema, serikali haitasahau mchango wa marehemu Dilunga enzi za uhai wake, kwamba aliitumia vyema kalamu yake katika tasnia ya habari kutetea masilahi ya taifa lake.

Dk. Mwakyembe amesema, kutokana na mchango wake Dilunga kwa taifa enzi za uhai wake, Rais John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa wametuma salamu zao za rambirambi.

“Pamoja na kwamba wizara imewakilishwa hapa, nilikuwa na kikao cha dharura lakini nimelazimika kuja hapa kutokana na mchango wake.

“Kutokana na umuhimu wake, rais, makamu wa rais na waziri mkuu wamenituma kuja kutoa salamu zao za rambirambi,” amesema Dk. Mwakyembe.

Nevil Meena, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amesema, jukwaa hilo limepata pigo kwa kuondokewa na hazina kubwa.

“Leo ni siku ya majonzi makubwa kwa wanatasnia ya habari, leo tunaomboleza kifo cha hazina kubwa ya jukwaa letu. TEF ilikuwa ni taasisi aliyoiheshimu na kuithamini,” amesema Meena.

Akisoma wasifu wa marehemu, Deudatus Balile, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampeni ya Jamhuri Media, amesema Dilunga alianza kupata matatizo ya afya mwezi Julai mwaka huu, ambapo alianza kulalamika kusumbuliwa na maumivu ya tumbo.

Balile ameeleza kuwa, tarehe 15 Agosti mwaka huu Dilunga alifanyiwa vipimo katika Hospitali ya Kimara na kubainika kuwa na maradhi ya Typhoid na Malaria, na kuwa alitumia dawa pasina mafanikio.

Bada ya matibabu hayo kutofanikiwa, Dilunga alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala tarehe 1 Septemba 2019 na kuhamishiwa Muhimbili tarehe 10 Septemba mwaka huu alikopatiwa matibabu hadi umauti ulipomkuta tarehe 17 Septemba.

Balile amesema, marehemu Dilunga ameacha watoto watatu na mjane mmoja.

Mwili wa Dilunga umeagwa na watu wa kada mbalimbali ikiwemo wanasiasa na wanahabari, wakiongozwa Dk. Mwakyembe; Dk. Hassan Abassi, Msemaji Mkuu wa Serikali; Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu na Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje Mstaafu.

Wengine ni Nape Nnauye, Mbunge wa Mtama; Amina Molel, Mbunge Viti Maalum pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za habari hapa nchini.

Baada ya kuagwa, mwili wa Dilunga unasafirishwa kuelekea mkoani Morogoro kwa ajili ya shughuli ya mazishi itakayofanyika Ijumaa tarehe 20 Septemba 2019.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Askari Polisi wa wanawake watakiwa kuchangamkia fursa za elimu

Spread the love  KAMISHNA wa Polisi Utawala Menejimenti ya rasilimali watu, CP...

Habari Mchanganyiko

Vijana 400 waguswa na programu ya “Learning for Life” ya SBL

Spread the love  PROGRAMU ya “Learning for Life” imetimiza dhamira ya Serengeti...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Stamico yafungua fursa za kiuchumi kwa makundi maalumu

Spread the loveSHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limemwaga neema kwa watu...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Maabara ya bilioni 5 upimaji madini yazinduliwa Geita, inapima kwa mionzi

Spread the loveZaidi ya Sh bilioni tano zimewekezwa katika kampuni ya MSALABS...

error: Content is protected !!