May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Diamond ashindwa BET na Burna Boy, atoa ujumbe

Burna Boy

Spread the love

 

MSANII wa Nigeria, Burna Boy ameibuka mshindi wa tuzo ya BET 2021 kama msanii bora wa kimataifa na kuwaangusha wasanii wengine akiwemo, Diamond Platinum wa Tanzania. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Tuzo hizo, zimetolewa usiku wa kuamkia leo Jumatatu, tarehe 28 Juni 2021, katika ukumbi wa Microsoft mjini Los Angeles, nchini Marekani.

Wengine waliokuwa wakiwania tuzo hiyo ni; Aya Nakamura (Ufaransa), Emicida (Brazil), Headie One (Uingereza) na Wizkid (Nigeria), Young T na Bugsey wa Uingereza pamoja na Youssopha wa Ufaransa.

Mara baada ya kushindwa kwenye tuzo hizo, Diamond ametumia ukurasa kwake wa Instagram kuzungumzia tuzo hizo akisema “kupitia tuzo hii nimeona ni kiasi gani Watanzania tuna umoja, upendo na kuthamini vya kwetu…”

Naseeb Abdul ‘Diamond Platinum’

“Nawashkuru sana kila mmoja wenu kwa upendo mkubwa mlionionesha… Ni faraja kuona Dunia inapotaja nchi zenye wanamuziki bora Tanzania inatajwa, ni jambo la kumshukuru Mungu.”

“….na naamini wakati mwingine tutaibeba… nitafarijika kesho na kesho kutwa msanii mwingine pia akiwa katika jambo la kuwakilisha taifa tumpe nguvu kama mlionipa…. sis ni #SwahiliNation sisi ni Taifa la Waswahili,” amesema Diamond.

Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa naye ameambatanisha video ya Diamond akiwa viunga vya ukumbi zilipotolewa tuzo na kuandika “hatukupata tuzo lakini tumeongeza heshima.”

“Kudos @diamondplatnumz Watanzania tunajua wewe ni mshindi, mpambanaji, mzalendo wa kweli na mwanamuziki bora sana Afrika na Duniani.”

“Tutaipata wakati mwingine. Thanks #betawards for nomination. Aluta continua…,” amesema Msigwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari- Maelezo.

Tangu BET ilipotoa orodha ya wanaowania tuzo hizo, ikiwemo ya Diamond, wadau wa haki za binadamu nchini Tanzania, walipinga uteuzi wake.

Katika kushinikiza BET inamwengua kwenye kinyang’anyiro hicho, mtandao wa Change.org ilikusanya saini za watu mbalimbali ili kushinikiza waandaaji wa tuzo hizo kumtoa na zaidi ya saini 22,000 zilisainiwa.

Diamond alikwenda kushiriki tuzo hizo huku kukiwa na baadhi ya Watanzania waliopinga kutajwa kuwania tuzo hizo kwa madai kwamba, hakuwa miongoni mwa wasanii waliopinga ukiukwaji wa utawala bora.

Mwanamuziki mkongwe wa Rap na Muigizaji Queen Latifa raia wa Marekani, amekabidhiwa tuzo ya maisha 2021 kutokana na ufanisi wa kazi zake.

error: Content is protected !!