August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dhoruba ya Seif yamtikisa IGP, Dk. Shein

Spread the love

MGOGORO wa kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) visiwani Zanzibar unazidi kufukuta, anaandika Faki Sosi.

Serikali ya Dk. Ali Mohamed Shein, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar inatikiswa na dhoruba kali kutoka kwa Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa CUF.

Sasa serikali inayoongozwa na CCM inapanga kumfikisha mahakamani Maalim Seif kwa madai ya kuwepo kwa mtukio mbalimbali ya kihalifu yanayotokana na sababu za kisiasa visiwani humo.

Ispekta Jenerali Ernest Mangu, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini wakati akizungumza na Kituo cha Televisheni cha Azam jana amesema ‘tutamfikisha mahakamani Maalim Seif wakati wowote kuanzia sasa.’

Kuna mtikisiko mkubwa visiwani humo kutokana na Serikali ya Dk. Shein kususwa na wananchi wake kwa madai ya kuwepo madarakani kwa njia haramu.

Mara kadhaa viongozi wa CCM visiwani Zanzibar wamekuwa wakilalamika kuwa, wafuasi wao wanakabiliwa na mazingira magumu kutoka kwa wafuasi wa CUF huku wakiihusisha hali hiyo na Maalim Seif.

Miongoni mwa matukio makubwa yanayoripotiwa kufanyika visiwani humo ni kuvamiwa kwa wananchi na kukamatwa kuteswa na ‘mazombi’ huku CCM na CUF wakisukumiana kuhusika na vitendo hivyo.

Tayari CUF kupitia Salim Bimani, Makurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho amelitaka Jeshi la Polisi kupeleka ushahidi wake unaohusu chama hicho kuhusika na matukio ya uhalifu katika vyombo vya kimahakama.

IGP Mangu amesema kuwa, Maalim Seif amekuwa akiwachochea wafuasi wake waichukie Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kuwa, wamekuwa wakifyeka mazao kwenye mashamba kisiwani Pemba.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa, ilitanguliwa na wenye maduka kubagua wateja wa kuwauzia bidhaa, wamiliki wa magari ya usafiri kubagua abiria na hata kwenye misiba kubaguana kwa misingi ya itikadi za vyama.

Kasi ya vitendo hivyo imekua zaidi baada ya uamuzi hasi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana na kupanga uchaguzi mpya uliofanyika tarehe 20 Machi mwaka huu.

Kwenye uchaguzi huo (Machi 20), Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa ZEC pia kada wa CCM alimtunuku Dk. Shein urais wa visiwa hivyo baada ya CUF na baadhi ya vyama vya upinzani kususia uchaguzi huo.

IGP Mangu anasema kuwa, kabla ya uchaguzi wa Oktoba mwaka jana na ule wa Machi mwaka huu, visiwa hivyo vilikuwa tulivu na kwamba, hakukuwepo na viashiria vyovyote vya vurugu.

Mkuu huyo wa polisi amesema kuwa, awali wakati Maalim Seif akifanya vikao vya ndani hawakuona tatizo lolote na kudai kuwa, kwenye vikao hivyo alikuwa akifanya uchochezi.

Maalim Seif siku za hivi karibuni alikuwa akifanya mikutano ya ndani ya wanachama pia viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho.

Miongoni mwa mazungumzo yaliyowahi kuripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na Mwanahalisionline ni kuwa, aliwataka viongozi na wanachama wake kumsusia visiwa hivyo Dk. Shein.

Pia Maalim Seif alieleza kuwa, Wazanzibari walimchagua yeye na si Dk. Shein huku akisisitiza kuwa, haki ya raia wa visiwa hivyo itapiganiwa kwa njia ya amani.

error: Content is protected !!