September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Dhoruba ya mauaji yatia hofu

Spread the love

SERIKALI ya Rais John Magufuli inakumbwa na mtikisiko wa mauaji kutokana na matukio hayo kufanyika mfululizo, anaandika Wolfram Mwalongo.

Wakazi wa Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima katika Manispaa ya Tanga wameingia hofu kutokana na wenzao kuvamiwa na kuuawa kwa kuchinjwa na kisha wauaji kutokomea pasipo kukamatwa.

“Tumeingia mashaka, hali ya hapa si nzuri hata kidogo. Usalama wetu upo mashakana na bila shaka watu hawa watarudi siku za baadaye,” anasema Asha Salum, Mkazi wa Mzizima.

“Tuka mauaji yatokee juzi, hakuna hata mmoja aliye na amani hapa. Tupo na usiku siku hizi tunauona mrefu, sijui nini kimetokea hapa kwetu,” anazungumza Frederick Samson.

Usiku wa kuamkia jana watu wanne wameuawa kwa kuchinjwa wakiwemo watatu kutoka katika familia moja.

Kwa mujibu wa Leonard Paul, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, tukio hilo lilitokea majira ya saa saba usiku kwenye Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima katika Manispaa ya Tanga.

Waliokufa kwenye tukio hilo ni Issa Hussein (50) Mkola Hussein (40) Hamisi Issa (20) na Mikidadi Hassan (70).

Wengine ni raia wa Kenya waliofahamika kwa jina moja  Mahmoud mwenye umri kati ya Miaka 35 na 40, Issa Ramadhan (25) pamoja na wachunga Ng’ombe wawili waliofahamika kwa jina moja Kadiri na Salum.

Kwa mjibu wa mashuhuda wa tukio hilo wamesema, wahusika wa uhalifu waliwalazimisha kufungua milango usiku kabla ya kuwaua.

Kamanda Paul,  majambazi hao walivamia nyumba ya Mkola, nyumba ya Mikidadi  na kuwachinja kabla ya kumalizia nyumbani kwa Issa.

“Watu hao walivamia nyumba hizo tatu na kuanza kuua kwa kutumia mapanga na visu,”amesema Kamanda Paul.

Amesema, walianza kuvunja nyumba ya kwanza na kukuta watu watatu ambao waliwaua wote kwa kuwakata maeneo mbalimbali ya mwili.

“…, kisha kuvamia nyumba ya pili na tatu na kufanya hivyo hivyo. Baada ya kufanya mauaji hayo waliiba mchele, sukari na biskuti na kutokomea navyo msituni karibu na maeneo ya Amboni,” amesema Kamanda Paul.

Tukio hilo ni miongoni mwa matukio ya kutisha yalikitanguliwa na tukio lililotokea Sengerema, Mwanza ambapo watu saba wakiwemo watano wa familia moja kuuawa kwa kunyongwa.

Wiki moja baadaye ndani ya Msikiti wa Rahma ‘Masjid Rahma’ mkoani Mwanza mauaji yalitokea ambapo watu watatu waumini wa msikiti huo walipoteza maisha baada ya kuvamkiwa wakiwa katika swala ya saa mbili (Isha).

 

error: Content is protected !!