July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Dhibiti uhalifu Afrika msiende ICC’

Spread the love

VIONGOZI wa nchi za Afrika wawe tayari kushughulikia masuala ya uvunjaji wa haki za binadamu, ikiwemo mauaji ya kupanga ya raia, iwapo wana msimamo wa kutoitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ya The Hague (ICC). Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Rai hii ameitoa Kamishna wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Muhammad Yussuf Mshamba wakati wa Kongamano la Wazi kuhusu Maadili katika Kuimarisha Amani, Umoja na Haki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF).

Mshamba amesema Taifa linapoingia katika uchaguzi mkuu kupata viongozi wenye ridhaa ya wananchi, linapaswa kuangalia kwa makini umuhimu wa watendaji wa asasi zinazosimamia uchaguzi kuzingatia sheria na kanuni ili kuepusha chuki ambayo ndio chanzo cha mauaji yanayolazimu kushughulikiwa na ICC.

Amesema mahakama ya ICC iliyoko The Hague, nchini Uholanzi, ni ya kisheria iliyoanzishwa kwa ridhaa ya mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa, ambayo inashughulikia makosa yaliyofanywa na tawala zilizo madarakani au waasi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

“Lakini kama hatuzitaki basi maana yake sisi wenyewe tuoneshe moyo wa kujizuia na kutenda makosa mabaya au yanapotokea tutumie mahakama zetu kuyadhibiti kwa kuwashughulikia waliohusika,” amesema.

Ametolea mfano wa Rwanda iliyoanzisha mahakama zake za Gachacha kushitaki waliotuhumiwa kushiriki mauaji ya halaiki mwaka 1994, kusaidia Mahakama ya ICTR iliyokuwa Arusha; Sierra Leone ilimshitaki Charles Tailor wa Liberia, baadaye ndio akakabidhiwa The Hague; na Hisne Habre aliyekuwa Rais wa Chad, anashitakiwa sasa na mahakama iliyoko nchini Senegal.

Mshamba amesihi viongozi wa kisiasa kuacha kutoa kauli nzito zisizofaa ambazo hutosha kuzusha matatizo ambayo hatimaye ndio huchochea machafuko.

Amegusia hilo akitaja kauli ya “Goli la Mkono” iliyotolewa na Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, akielezea kwamba chama chao kitashinda tu uchaguzi ujao hata kwa lazima.

Kauli nyingine ni inayotolewa na viongozi wa CCM Zanzibar kwamba “Serikali ya Mapinduzi haiwezi kutolewa kwa vikaratasi, wakiitaka labda nao wapindue kama tulivopindua mwaka 1964.”

Neno “vikaratasi” linamaana kuwa njia ya kufanya uchaguzi wa kidemokrasia kwao CCM haiwezi kuzingatiwa katika kukabidhi madaraka ya serikali Zanzibar kwa chama cha upinzani.

error: Content is protected !!