Monday , 27 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kuporwa mafao ya Wafanyakazi, dhambi ya Bunge au tunalishwa matango pori?
Habari za Siasa

Kuporwa mafao ya Wafanyakazi, dhambi ya Bunge au tunalishwa matango pori?

Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema
Spread the love

WAKUBWA zangu salaam. Mimi ni Mbunge na kwa hiyo ninaweza kusemwa nina maslahi katika mjadala huu. Ninayo kweli. Anaandika Tundu Lissu, Ubelgiji … (endelea).

Kwa vile ‘mmetupiga’ sana kwenye suala hili, ninaamini hamtajali sana nikijitetea mwenyewe, na kuwatetea wenzangu, hata kama hawajanituma.

Kuna hatari kubwa ya kutumia suala la mafao ya wafanyakazi kuwachonganisha Wabunge kwa wananchi, ili watu wenye agenda za kuua Bunge letu kama taasisi watimize matakwa yao. Naomba kufafanua.

Ni kweli kwamba utaratibu huu wa mafao hauwahusu Wabunge. Lakini sio Wabunge peke yao. Utaratibu huu hauwahusu pia Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote. Vile vile hauwahusu Mawaziri na Naibu Mawaziri wote, Rais na Makamu wa Rais.

Hawa wote sio ‘wafanyakazi’ kwa maana ya kisheria ya neno hilo. Ni watumishi wa kisiasa na mishahara na marupurupu yao yapo kwenye kundi la utumishi wa umma wa kisiasa.

Na sio wanasiasa tu ambao sio ‘wafanyakazi.’ Makamishna wa Tume mbali mbali zilizoanzishwa kwa mujibu wa Katiba au sheria mahsusi, na wajumbe wa Bodi mbali mbali za taasisi na mashirika ya umma nao sio ‘wafanyakazi’, na kwa hiyo hawahusiki na utaratibu huu wa mafao ya wafanyakazi.

Wote niliowataja hawalipwi pensheni wanapomaliza muda wao wa utumishi. Hulipwa kitu kinaitwa ‘gratuity’ (mtanisaidia Kiswahili chake), yaani malipo ya mkupuo mmoja wanapomaliza utumishi.

Viwango vya gratuity hiyo vinatofautiana kulingana na cheo cha mhusika. Kwa Wabunge mnaotusema sana ni 40% ya mishahara yote ya miaka mitano. Hicho pia ni kiwango cha Wakuu wa Wilaya ambao hamjawagusa kabisa kwenye mjadala huu.

Kwa Wakuu wa Mikoa na Naibu Mawaziri, gratuity yao ni 50% ya mishahara yote ya muda wao utumishi. Hawa pia hakuna anayewasema.

Kwa Mawaziri (na kama sikosei Naibu Spika) kiwango cha gratuity yao ni 60% ya mishahara yote ya muda wao wa utumishi. Hapa pia sijasikia malalamiko wala hasira yoyote.

Kwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Spika, hawa utaratibu wao ni mnono zaidi. Kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Viongozi wa Kisiasa ya mwaka ’99, Rais anayemaliza muda wake anatakiwa kulipwa 80% ya mishahara yote ya Urais wake; mshahara wake wote wa miaka miwili kwa ajili ya maandalizi ya kustaafu; na baada ya hapo ataendelea kulipwa 80% ya mshahara wa Rais aliyeko madarakani hadi atakapofariki dunia.

Mafao haya ni nje ya mafao mengine kama nyumba yenye furniture zote, magari, ofisi, walinzi na watumishi kadhaa wa ndani na wa ofisi. Sijaona wala kusikia mtu yeyote akimnyooshea kidole mtetezi wa wanyonge aliyeko Magogoni kwa sasa, wala kuhoji uzalendo au uadilifu wake.

Kwa Makamu wa Rais kiwango ni hicho hicho cha 80% ya mishahara yote na baada ya hapo pensheni ya kila mwezi ya 80% ya mshahara wa Makamu wa Rais aliyeko madarakani hadi kifo. Na hii pia ni nje ya nyumba, furnishings, gari, walinzi, watumishi, etc.

Kwa Waziri Mkuu na Spika ni 70% kwa utaratibu huo huo.

Ukiachia Wabunge, hakuna yeyote ambaye amewalalamikia wote hawa, pamoja na ukweli kwamba mafao yao ni makubwa kuliko ya Wabunge.

‘Ignorance is bliss’, Waingereza wanasema. Ujinga ni amani. Watu wetu wengi ni wajinga, hawaelewi nchi hii inavyoendeshwa. Kwa hiyo ni warahisi sana kuaminishwa kwamba Wabunge wao ndio wabaya, wasaliti, etc.

Wakishaamini kwamba Wabunge ndio tatizo, itakuwa rahisi zaidi kujenga hoja za kulidhoofisha Bunge letu zaidi ya lilivyo sasa. Tayari Serikali ya Magufuli imefanya na inaendelea kufanya mambo mengi yenye kulidhoofisha Bunge letu.

Je, nitahojiwa, Wabunge si ndio waliopitisha sheria hii ya kuwanyonga wafanyakazi na kujipendelea wao na wakubwa wenzao???

Jibu la haraka haraka ni ndio, sheria hiyo, na hizo nyingine zimepitishwa na Bunge.

Lakini suala la msingi ni je, kwa Katiba yetu ya sasa na Sheria zake, na kwa historia yetu ya kisiasa na ya kibunge ya tangu Uhuru, Wabunge hawa walikuwa na uwezo wa kukataa kupitisha sheria hizi???

Angalau tangu Katiba ya Jamhuri ya mwaka ’62, Bunge la Tanganyika, na baadae Tanzania, limeendeshwa, kwa kiasi kikubwa, na Ikulu.

Bunge la mpaka mwaka ’85 liliendeshwa na Ikulu ya Mwalimu Nyerere; la mpaka mwaka ’95 liliendeshwa na Ikulu ya Mzee Mwinyi; la mpaka mwaka ’05 lilikuwa kwenye mabawa ya Ikulu ya Ben Mkapa; la hadi mwaka ’15 lilikuwa chini ya kivuli cha Ikulu ya Jakaya Kikwete, na Bunge la sasa liko chini ya udhibiti mkubwa wa Ikulu ya Magufuli. Huu ndio ukweli mchungu wa historia ya nchi yetu.

Kwa miaka yote hii, kwa sababu ya kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme, Bunge letu limekuwa dhaifu sana. Bunge la aina hii, haliwezi – na halijawahi – kukataa Muswada unaopelekwa Bungeni na Ikulu. The very few, if any, exceptions only prove the general principle of our history.

Kwa hiyo, kuwalaumu Wabunge hawa kwa kupitisha sheria hii ya mafao ya wafanyakazi is simply to miss the point. Bunge la kondoo la miaka yote hii haliwezi kubadilika ghafla na kuwa Bunge la simba!!!

Nataka niwe wazi. Hapa ninazungumzia Bunge la wanaCCM. Sisi wapinzani tumekuwa wachache miaka yote hii tokea mwaka ’95. Tumekuwa tunapinga mambo haya lakini, kwa sababu ya uchache wetu, ‘tumefyekelewa mbali’ na wale wanaosema: “Wanafiki waseme NDIYO!!!”

Na wanafiki wamesema ‘NDIYO’ kwa kila kitu walicholetewa na Ikulu ya Mwenyekiti wao wa Chama. Kwa hiyo, Sheria hii ya mafao ya wafanyakazi ni Sheria ya mpangaji wa sasa wa Ikulu pamoja na Wabunge wa Chama chao. Hili ni la kwanza.

La pili, na la mwisho kwa leo, linahusu sababu halisi ya mabadiliko haya ya sheria za mafao ya wafanyakazi.

Sababu halisi sio uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi wanaostaafu kama tunavyoambiwa na Mifuko yenyewe, au wakubwa wa Serikali hii. Hayo ni ‘matango pori’ wanayolishwa the blissfully ignorant.

Sababu halisi ni kwamba watawala wa CCM wameua mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kutapanya pesa za wafanyakazi kwenye miradi isiyokuwa na tija kwa wafanyakazi.

Pesa za wafanyakazi zimetumika kujenga ‘White Elephants’ kama majengo mengi na makubwa yaliyopo Dar Es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na kwingineko.

Kwa kiasi kikubwa, na kwa sababu mbali mbali, majengo haya hayapangishiki. Hivyo, licha ya kugharimu matrilioni ya shilingi, fedha za wafanyakazi hazitarudi.

Mifuko ya hifadhi ya jamii ndiyo iliyojenga UDOM; na tangu mwaka ’09 CAG amelalamika kwamba Serikali imeshindwa kurudisha fedha hizo za wafanyakazi kwa sababu ama hakukuwa na mikataba au mikataba yenyewe haieleweki.

Pesa za wafanyakazi ndizo zilizojenga Ofisi ya Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi karibu na St. Peter’s, Dar Es Salaam; nyumba za polisi Kurasini Dar; Machinga Complex Dar; Daraja la Kigamboni Dar, n.k.

Pesa za wafanyakazi zimetumika sana kuhonga baadhi ya Mawaziri na Wabunge kwa kuwapa miradi inayoitwa ya maendeleo, kama vile kununua mipira na jezi za michezo kwa timu za vijana kwa majimbo ya Wabunge na Mawaziri hao.

Waliofaidika na ‘ukarimu’ huu ni pamoja na Rais Magufuli mwenyewe, akiwa Waziri na Mbunge wa Chato. Hili nililizungumzia hata Bungeni takriban miaka minne iliyopita.

Lengo la hongo hizi ni kuwanyamazisha ili watu ‘wapige’ pesa za wafanyakazi. Ndio maana wala sio ajabu kwamba waliokamatwa na kushtakiwa kwa ‘kupiga’ pesa za mifuko ya hifadhi ya jamii sio akina Ramadhani Dau au Sanga wa iliyokuwa NSSF na LAPF, au akina AG Masaju na Naibu Spika Tulia Ackson waliokuwa Wadhamini wa Mifuko hiyo, bali ni wakurugenzi na mameneja wa kati wa Mifuko.

Wakurugenzi Wakuu na Wadhamini wa Mifuko, waliofanya maamuzi ya utapanyaji huu wa fedha za wafanyakazi, wamepandishwa vyeo na kuwa mabalozi au wabunge wa kuteuliwa na Rais au Majaji wa kuteuliwa na Rais pia.

Baada ya kuifilisi mifuko ndio watawala wakaanzisha hizi hoja za mara kuiunganisha, mara kubadili mfumo wa mafao, etc.

Suala muhimu lisilozungumzwa ni je, mifuko hii ina fedha za kulipa wafanyakazi wanaostaafu au kuacha kazi kwa sababu mbali mbali??? Pesa ‘zilizokopwa’ kujengea miradi hii na mingine mingi zimerudishwa lini?

Naomba kumalizia. Kutupiga Wabunge ni sawa sawa. Bunge lina sehemu yake ya lawama kwenye hili. Lakini ni Bunge peke yake??? Kwa utaratibu halisi wa utungaji sheria wa nchi yetu chini ya Katiba ya sasa, Bunge ndio lenye mamlaka haya yanayosemwa??? Mjadala na uendelee.

Mwandishi wa makala hii, Tundu Antipas Lissu, ni mbunge wa Singida Mashariki. Kwa sasa, yuko Tienen, Belgium anakopatiwa matibabu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kasekenya aipa Tanroads wiki kukarabati barabara Morogoro

Spread the loveNaibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ametoa wiki moja...

Habari za SiasaTangulizi

‘Aliyemtonya’ Lissu kuhusu rushwa arejea madarakani

Spread the loveMwenyekiti wa zamani wa Chadema Mkoa wa Iringa, William Mungai...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Tutaendelea kupigania malengo ya afrika

Spread the loveRais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema dhamira ya Tanzania...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NHC yadai bil. 2.1 taasisi za Serikali, Waziri atoa maagizo

Spread the loveKAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii...

error: Content is protected !!