July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Deo Filikunjombe buriani

Spread the love

ALIYEKUWA mbunge wa jimbo la Ludewa ambaye anatetea kiti hicho katika uchaguzi wa Oktoba 25, Deo Filikunjombe amefariki dunia katika ajali ya helikopta. Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Pia Kapteni William Silaa, aliyekuwa akirusha helikopta hiyo, ikitokea uwanja wa Dar es Salaam kwenda jimboni Ludewa, mkoani Iringa, pamoja na mdogo wa Filikunjombe, aitwaye Haule, pia wamefariki dunia katika ajali hiyo.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, Filikunjombe alikuwa katika msafara wa kwenda jimboni kwake kukamilisha ngwe ya mwisho ya kampeni.

Taarifa za mapema za ajali hiyo zimetangazwa na Jerry Silaa, ambaye ni mtoto wa Kapteni Silaa aliyefariki dunia katika ajali hiyo. Silaa aliandika katika akaunti yake ya mtandao wa picha, Instagram, akisema ajali imemhusisha baba yake ambaye ni rubani.

Taarifa za ajali hiyo zilianza kuenea tangu jioni jana lakini mpaka mchana alasiri hii, Jeshi la Polisi limeshindwa kutoa taarifa rasmi inayoonesha majina yote ya waliokuwa kwenye helikopta hiyo wala kutaja kampuni inayoimiliki.

Kituo cha televisheni cha ITV kiliwasiliana kwa simu na Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi nchini, Paul Chagonja, akimuuliza undani wa tukio hilo lakini ameshindwa kujibu hoja hizo.

Angalau Kamishna Chagonja alisema helikopta hiyo ilianguka usiku wa kuamkia leo eneo la Pori la Hifadhi ya Selous, ukanda wa Rufiji mkoani Pwani.

“Mtu aliyeiona ametoa taarifa kuwa ilianguka lakini hatujafanikiwa kupata uhakika wa taarifa kuwa iliungua ilipofika chini… helikopta imesajiliwa kwa Na. 5Y-DKK,” alikaririwa akisema Kamishna Chagonja.

Silaa ambaye baba yake amekufa katika ajali hiyo alichapisha taarifa ya kuarifu tukio hilo akisema, “nimepokea taarifa kutoka kwa timu ya uokoaji kuwa abiria wote waliokuwa kwenye helikopta hiyo wamefariki dunia akiwemo Baba yangu mzazi na rafiki yangu Deo Filikunjombe.”

Kwa kawaida, hakuna ndege inayoondoka uwanjani, hata iwe ndogo kiasi gani, lazima inakuwa na orodha ya watu waliosafiri (manifesto). Wala hakuna kitu kama haijulikani mmiliki wake.

Ajali hiyo inasababisha kukata roho kwa mgombea wa sita wa ubunge baada ya Dk. Emmanuel Makaidi wa National League for Democracy (NLD), aliyekuwa akigombea jimbo la Masasi mkoani Mtwara, kufariki jana mchana baada ya kuugua ghafla nyumbani kwake Masasi mjini.

Filikunjombe alikuwa mbunge kutoka Oktoba 2010. Kabla ya Dk. Makaidi, walioaga dunia na majimbo yao kwenye mabano ni Dk. Abdallah Kigoda (Handeni mjini, CCM), Estomii Mallah (Arusha mjini, ACT-Wazalendo), Celina Kombani (Ulanga Mashariki, CCM) na Mohamed Mtoi (Lushoto, Chadema).

Uchaguzi wa majimbo hayo umeahirishwa katika majimbo hayo hadi mwezi ujao.

error: Content is protected !!