August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Denti’ wa ngono atozwa faini 200,000

Mhandisi Mathew Mtigumwe, Mkuu wa Mkoa wa Singida

Spread the love

ZUBERI Manjemi, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Manyoni mkoani Singida amemtoza faini ya Sh. 200,000 mwanafunzi wa kike wa Darasa la Nne kwa madai ya kufanya ngono, anaandika Mwandishi Wetu.

Hatua ya mwenyekiti huyo kumtoza fedha binti huyo imezua mjadala Manyoni kwa madai, amekwenda kinyume na taratibu katika kukomesha tabia ya watu kufanya ngono na wanafunzi.

Hata hivyo, Mhandisi Mathew Mtigumwe, Mkuu wa Mkoa wa Singida ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani Manyoni, Singida kumkamata mara moja mwenyekiti Manjemi.

Mhandisi Mtigumwe ametoa agizo hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika Kijiji cha Rungwa, Tarafa ya Itigi, Manyoni baada ya mwananchi Ally Ramadhani kutoa malalamiko yake kwamba, Manjemi ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza la usuluhishi la kata hiyo kwenda kinyume na taratibu.

Akifafanua zaidi Ramadhani amesema kuwa, kitendo cha mwenyekiti huyo kumtoza binti adhabu ya faini ya Sh. 200,000 na kutokuchukua hatua zo zote za kisheria dhidi ya mkazi aliyekuwa akituhumiwa kuwa na uhusiano wa kingono na mwanafunzi huyo, hakikuwa sahihi.

“Mkuu wa Mkoa adhabu hii ya upande mmoja haivumiliki kabisa, kwani mwanaume ambaye alikuwa akimrubuni mwanafunzi wa kike kufanya naye mapenzi ameachwa huru bila kupewa adhabu yote yote ile,” amesema kwa masikitiko.

Mkuu wa mkoa huyo alipomtaka Manjemi kueleza sababu ya kumtoza faini binti alisema kwamba, alitoa adhabu hiyo kwa madai binti huyo alitenda kosa kwa kukubali kupokea simu ya kiganjani kutoka kwa mwanaume, ili waweze kufanikisha mawasiliano ya kimapenzi.

Hata hivyo, baada ya maelezo hayo ya utetezi, ndipo Mkuu wa Mkoa alipomuagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo kumkamata na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Haingii akilini eti mwanafunzi wa kike atozwe faini huku mtu aliyekuwa akimrubuni anaachwa bila kuchukuliwa hatua zo zote za kisheria,” amesisitiza Mhandisi Mtigumwe.

Mhandisi Mtigumwe amesema kuwa, serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha wanafunzi wa kike wanafikia ndoto zao za kielimu lakini baadhi ya wanaume wakiwemo viongozi,wamekuwa vikwazo dhidi ya juhudi za serikali.

Mtigo ulivyokuwa; Baada ya walimu wa Shule ya Msingi Rungwa kutilia wasiwasi kuhusu umiliki wa simu ya mkononi ya mwanafunzi huyo, walimuhoji ambapo binti huyo alikiri kuhongwa.

Kisha walimu hao walimtaka mwanafunzi huyo kumpigia simu aliyempa simu hiyo ili kusikiliza mwenendo wa mazungumzo yao.

Mwanafunzi alifanya kama alivyoagizwa na walimu wake na ndipo walipobaini mwanaume huo kupokea na kuzungumza maneno ya mahaba kwa mwanafunzi huyo.

Baada ya hapo walimu hao walichukua namba ya simu ya mwanaume huyo na kuifikisha katika Baraza la Kata kwa hatua zaidi.

error: Content is protected !!