April 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Dengue, Vitambi vyazua mjadala bungeni

Spread the love

TATIZO la vitambi na mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Dengue, umezua mjadala bungeni kufuatia wabunge kadhaa kuhoji mpango wa serikali katika kudhibiti matatizo hayo. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Nape Nnauye, Mbunge wa Mtama leo tarehe 29 Mei 2019 akiwa bungeni jijini Dodoma, amehoji serikali kwamba inachukua hatua gani kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa homa ya dengue ili kuepusha vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

“Serikali inajitahidi kupambana na magonjwa mbalimbali, hivi karibuni kuna ugonjwa wa Dengue na umeanza kuripotiwa vifo.  Serikali inachukua hatua gani kuudhibiti sababu sipodhibitiwa watu wanazidi kuuawa,” amesema Nape.

Akijibu swali hilo kwa niaba ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Abdallah Ulega, Naibu Waziri wa Uvuvi na MIfugo amesema serikali inachukua hatua mbalimbali kukabiliana na athari za ugonjwa huo ikiwemo kuhakikisha matibabu yake yanatolewa kwa gharama nafuu.

“Ni kweli kuwa hapa karibuni kumeibuka ugonjwa wa Dengue hasa mkoa wa Dar, serikali imeanza kuchukua hatua za makusudi, naomba niwahakikishie moja ya mambo ambayo serikali imegundua ni kuwa, wananchi wamekuwa wakitumia gharama kubwa kwenye vituo vya huduma ya afya, serikali imehakikisha matibabu yanapatikana kwa bei nafuu ili kusaidia Watanzania,” amesema Ulega.

Awali, mjadala wa vitambi ulianzishwa na Mbunge Viti Maalum, Khadija Nasri Ally, aliyehoji kwamba serikali inafanya nini kukabiliana na tatizo la uzito uliokithiri ikiwa ni pamoja na kuongezeka vitambi ambapo ni dalili ya magonjwa yasiyoambukiza, huku akiitaka kueleza mbinu za kitaalamu katika kupambana na changamoto hiyo.

‘Uzito mkubwa wa mwili ni dalili ya magonjwa ya kuambukizwa, serikali inafanya nini kukabiliana na hili?  Mbali na mazoezi mbinu gani nyingine za kitaalamu za kupambana na vitambi?” Amehoji Khadija.

Swali hilo lilimsukuma Spika wa Bunge, Job Ndugai kutoa nafasi kwa wabunge wenye vitambi kuuliza maswali mbalimbali kuhusu tatizo hilo ili serikali itoe majibu.

“Jamani nyongeza ziwe za wenye vitambi, sasa niangalie wenye vitambi wasiokuwa na vitambi hawana ruhusua ya kuuliza maswali,” amesema Spika Ndugai.

Mbunge wa Njombe Kusini, Edward Mwalongo ameuomba uongozi wa Bunge kuhakikisha mgahawa wa Bunge unatoa vyakula ambavyo havisababishi vitambi.

Mwalongo amedai kuwa, wabunge wengi hupata vitambi kutokana na mgahawa huo kuuza vyakula vinavyosababisha vitambi.

“Mimi sina kitambi nina mwili mkubwa, na nashukuru kwa maelezo ya naibu waziri, lakini kwa sisi wabunge chanzo ni kantini yetu, serikali iko tayari kuipa ratiba ya vyakula ili iandae vyakula vinavyostahili?” amehoji Mwalongo.

Akizungumzia kuhusu ombi hilo la Mwalongo, Spika Ndugai amesema uongozi wa bunge utalifanyia kazi na kuwataka wabunge kupendekeza aina za vyakula ambavyo wanataka mgahawa huo uandae.

“Hili ombi,  na ninaomba wabunge waandike karatasi inayopendekeza menyu,” amesema Spika Ndugai.

Waziri Ulega amesema, serikali imefanya mambo mbalimbali kuhakikisha inakabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kuanzisha kitengo cha kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.

Ulega amesema serikali inaendelea na utoaji elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali  ikiwemo elimu kuhusu ulaji wa vyakula vinavyofaa, mazoezi na viashiria vya hatari.

Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi ameitaka serikali kutoa ushauri kwa wananchi kuhusu aina za vyakula vinavyofaa ili waepukane na matatizo ya vitambi na uzito uliokithiri.

“Kwa kuwa hapa amebainisha wazi kwamba kitambi kinasababishwa na vyakula vilivyopitiliza na kwa utamaduni wetu vyakula vyetu ni vya wanga.  Serikali inatushauri tule vyakula gani, sasa hivi kuna changamoto ya vitambi kwa watoto kina mama, serikali ina mkakati gani mahsusi nini kifanyike ili lisiathiri makundi ambayo nimeyataja,” amehoji Shangazi.

Akijibu swali la Shangazi, Ulega amesema serikali inaendelea kuwashauri wananchi kuepukana na vyakula vya mafuta, unywaji pombe kupita kiasi ili kujiepusha na changamoto hiyo.

“Kitambi ni dalili moja wapo ya uzito kupita kiasi, hii si dalili njema na hupelekea magonjwa ya kuambukiza.  Njia bora ni kujikinga kutokukipata kwa kuzingatia ulaji wa chakula unaofaa na kufanya mazoezi.

Kuzingatia ulaji unaofaa, kupunguza kiwango cha wanga, sukari, chumvi na mafuta kwa chakula, kunywa maji na kupunguza unywaji pombe uliopitiliza,” amesema Ulega.

error: Content is protected !!