May 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

DED Sengerema asimamishwa kazi

Magesa Mafuru, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sengerema

Spread the love

 

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Magesa Mafuru, amesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo. Anaripoti Nasra Bakari, Dar es Salaam … (endelea).

Mafuru amesimamishwa kazi leo Jumanne tarehe 20 Aprili 2021, na Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Nteghenjwa Hosseah, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ummy amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, kuunda timu ya uchunguzi wa tuhuma hizo haraka.

Aidha, Ummy amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kuhakikisha mkoa wake unafuata   sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa fedha za umma.

Ummy Mwalimu, Waziri wa TAMISEMI,

“Aidha, Ummy amemuelekeza Mongella, kuhakikisha kwamba katika kipindi chote ambacho timu ya uchunguzi itakuwa ikifanya kazi katika halmashauri hiyo, malipo yote yatakayofanyika kuanzia sasa yazingatie sheria,” imesema taarifa ya Hosseah.

Ummy amechukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo kwenye halmashauri hiyo, zilizotolewa na Mbunge wa Sengerema Hamis Tabasamu na wananchi wa jimbo hilo.

“Tuhuma hizo zimeelekezwa kwa mkurugenzi mtendaji na baadhi ya wakuu wa idara hiyo, zinazoonyesha kuwa mkurugenzi kwa kushirikiana na wakuu wa idara hizo wamekuwa wakifanya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma,”imesema taarifa hiyo.

Taarifa ya Hosseah imesema, ubadhirifu huo umeathiri shughuli za utekelezaji wa miradi hiyo, kwa kiwango kilichokusudiwa.

error: Content is protected !!