KLABU ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dara es Salaam (DCPC), kimempongeza
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Leo Jumanne, tarehe 6 Aprili 2021, Rais Samia ameagiza wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo na wizara ya mawasiliano na teknolojia ya habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa.
Vyombo hivyo ni magazeti ya MwanaHalisi, Mseto, Tanzania Daima, Mawio na Kwanza TV.
Kutokana na agizo hilo, DCPC kupitia kwa Mwenyekiti wake, Irene Mark imesema,
imefurahishwa na kauli ya Rais Samia kuwataka watendaji wa wizara hizo kuacha kutumia mabavu wakati wa kufanya uamuzi badala yake watumie kanuni na sheria zilizopo.

“Sisi DCPC, tunaamini watendaji wa wizara ya habari ya utamaduni, sanaa na michezo, watayafanyia kazi kwa haraka maagizo ya Rais Samia na kurejesha ajira za wanahabari na wafanyakazi wa idara nyingine zilizopotea kwa kufungwa kwa vyombo vya habari,” amesema Irene
“DCPC tunaamini kwamba, sasa uhuru wa vyombo vya habari uliominywa kwa miaka kadhaa sasa unarejea. Pia, tunaiona azma ya Rais Samia ya kuongeza mawanda ya ukusanyaji wa kodi na kusaidia katika kuleta maendeleo ya nchi.”
Irene amesema “uamuzi huu wa Rais Samia, umekuja wakati muafaka kwani tasnia ya habari kwa miaka mitano ilipita kwenye wakati mgumu hali iliyosababisha kundi kubwa la wanahabari mahiri na makini kukosa kazi.”
Pia, DCPC imetia “wito kwa wanahabari kuendelea kufanyakazi zao kwa weledi na kuzingatia sheria ya uhuru wa vyombo vya habari ya mwaka 2016 na kanuni za utangazaji ili kufanyakazi kwa amani kwa kuwa tasnia ya habari ni mhimili wa nne wa dola.”
Leave a comment