MWANAHABARI Luqman Maloto, amefungua kesi ya jinai dhidi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu jijini Dar es Salaam, kwa kushindwa kuchunguza matukio yaliyofanywa na watu wasiojulikana. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msajili wa mahakama hiyo tarehe 11 Januari 2023, DCI na DPP wametakiwa kufika mahakamani hapo mbele ya Jaji John Nkwabi, tarehe 8 Februari mwaka huu, kwa ajili ya usikilizaji wa kesi hiyo ya Jinai No. 5/2023.
Leo tarehe 13 Januari 2023, MwanaHALISI Online imetamfuta kwa njia ya simu Wakili anayemuwakilisha Maloto katika kesi hiyo, Hekima Mwasipu, kwa ajili ya maelezo zaidi, ambapo amejibu akisema ni kweli mteja wake amefungua kesi hiyo.
Mtandao huu umemtafuta Maloto kwa njia ya simu ili kuzungumza naye kuhusu kesi hiyo, ambaye amesema mchakato wa kuifungua kesi hiyo ulianza 2022 lakini umekamilika 2023 kwa kupangiwa tarehe na jaji.
Maloto amedai kuwa, amefungua kesi hiyo ili mahakama itamke kwamba DCI ameshindwa kufanya kazi yake ya kuchunguza matukio hayo ikiwemo tukio la Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu, kushambuliwa na risasi Septemba 2017, akiwa jijini Dodoma.
“Tunachohitaji mahakama itamke kwamba DCI na DPP hawajafanya kazi yao inavyotakiwa au wameshindwa kufanya upelelezi wa matukio hayo kuhusu kupotea au kutoweka kwa Ben Saanane, mwandishi Azory Gwanda, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Simon Kanguye,”
“Tukio la Lissu kupigwa risasi na mauaji ya Akwiline Akwilini. Tunataka mahakama iseme DCI ameshindwa kufanya kazi yake ya upelekezi kuweza kusaidia Watanzania wajue nani amehusika na matukio hayo sababu ukiangalia watu ni wengi wametajwa na tumebaki dilemma hatujui kama nchi hatma ya hao watu ni nini na Watanzania tunapaswa kujua hatma yao,” amedai Maloto.
Kwa upande wa DPP, Maloto amedai kwamba “ameshindwa kwa nafasi yake kufungua mashtaka sababu angefungua tungeona kuna watu wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kumpiga risasi Lissu.”
Mwanahabari huyo amedai, mahakama endapo itatamka kwamba DCI na DPP wameshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, hatua nyingine za kisheria zitafuatwa.
“Safari moja huwa inaanzisha nyingine, sasa tunataka mahakama isaidie kutamka kwamba wameshindwa kazi baada ya hapo hatua nyingine itafuata. Lakini tumeona tuanzie hapo mahakama inasemaje kuhusu ukimya huu, sababu tunataka tujue polisi, DCI au DPP wako kazini au wameacha,” amedai Maloto.
Leave a comment