OFISI ya Mkurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchni Kenya imetangaza kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu madai ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kuwa kura zao za urais ziliibwa katika uchaguzi wa Agosti mwaka jana. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Katika taarifa iliyotolewa tarehe 25 Januari 2023, Mkurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Amin Mohamed alibainisha kuwa kitengo hicho cha polisi kimepokea malalamiko mengi kuhusiana na uchaguzi huo na kuikosoa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kuendesha uchaguzi na dosari.
Mohamed aliongeza kuwa anafahamu madai ya walalamikaji wanaodai kuwa kuna nakala rasmi ya matokeo ya urais ili kuhalalisha madai yao.
“Kwa maelezo, walalamikaji wanadai kuwa kuna hila mbalimbali zinazoashiria kughushi nyaraka na kughushi moja kwa moja nyaraka za mada,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
“Kwa njia ya kielelezo, wamebainisha madai mbalimbali ya ukiukwaji ikiwa ni pamoja na kutowiana dhahiri katika takwimu za alama zilizoangaziwa katika fomu zilizoandikwa kama 34B na ambazo zinapitishwa kama hati zinazotoka IEBC.”
Kwa hivyo, DCI akifanya kazi chini ya mamlaka ya kikatiba iliyopewa kitengo cha upelelezi, alibainisha kuwa timu yake itafanya uchunguzi kuthibitisha ukweli wa madai hayo.
“Kimsingi, ofisi ya DCI inaendelea na uchunguzi wa uhalali na uhalisia wa nyaraka husika, Pamoja na iwepo wa makosa yanayohusu kughushi nyaraka, yamefanyika chini ya Kifungu cha 345 – 348 cha Kanuni ya Adhabu,” alisema Mohamed.
IEBC pia imeombwa kuwasilisha fomu zao 34B zilizoidhinishwa zilizotumiwa kutangaza matokeo ya urais kwa makao makuu ya DCI, ili kusaidia katika uchunguzi huo.
“Kwa madhumuni ya kushughulikia kisheria malalamiko yaliyotajwa hapo juu kulingana na mamlaka yetu, tunaomba mtupe nakala zilizoidhinishwa za Fomu 34B ambazo zilitumika kujumlisha, kuthibitisha na kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais wa tarehe 9 Agosti 2022.”
Mapema wiki iliyopita baada ya kurejea kutoka ziara ya Afrika Kusini, kinara wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga aliwahutubia wafuasi wake katika uwanja wa Kamkunji jijini Nairobi ambapo aliwaarifu kuwa wao kama upinzani hawawezi kamwe kukubaliana na matokeo ya mwaka jana kwani yana hitilafu.
Odinga alisema hawawezi kumtambua William Ruto kama rais mteule wala serikali yake kwani ushindi wao haukuwa wa haki na kweli.
Leo Jumapili, Odinga anatarajiwa kutoa mwongozo zaidi kwa wafuasi wake katika mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika katika uwanja wa Jacaranda jijini Nairobi huku pia ikiarifiwa kuwa huenda atatoa mikakati ya kususia baadhi ya huduma na bidhaa zinazohusiana na serikali ya Ruto kama njia moja ya kuonesha malalamiko yao.
Hili lilikolezwa zaidi na kauli ya katibu wa chama cha Jubilee, Jeremiah Kioni alisema kuna mtoa taarifa wa kutegemewa kutoka IEBC ambaye amemfichulia nyaraka za kweli zinazoonesha kuwa Odinga alishinda uchaguzi huo kwa zaidi ya kura milioni nane.
Leave a comment