August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

DC Ukerewe aomba kivuko

Kivuko cha MV Ukara kikiwa kwenye safari zake

Spread the love

ESTOMIAH Chang’ah, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, ameiomba Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, kununua kivuko kipya kitakachotoa huduma ya usafiri kwa wakazi wa kisiwa cha Ukara wilayani humo, anaandika Moses Mseti.

Aprili 14 mwaka huu, kivuko cha MV Ukara kilizimika katikati ya Ziwa Victoria kikiwa na abiria kitendo ambacho kiliibua taharuki na hofu kubwa kwa abiria hao waliokuwa wakikitumia kusafiria kwenda katika kisiwa cha Ukara wilayani humo.

Chang’ah pia amesema badala ya kuendelea kutumia vivuko vya MV. Nyerere na MV Ukara ambavyo vimekuwa vikizimika ghafla mara kwa mara ndani ya Ziwa Victoria, kwa kutumia injini ambazo ni mbovu na badala yake wizara hiyo inapaswa kununua kivuko kipya.

Mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, alitoa ombi hilo kufuatia kuharibika kwa vivuko hivyo, vinavyotoa huduma ya usafiri wa abiria kati ya Bugorora na Ukara na kilichotaka kuhatarisha usalama wa abiria ndani ya Ziwa Victoria.

Amesema kuwa, kivuko cha MV Ukara, kilichokuwa kimebeba zaidi ya abira 100 na kuzimika ziwani, jambo ambalo alidai limemsukuma kuiomba wizara hiyo kununua kivuko kipya kitakachosaidia kutoa huduma wilayani humo.

“Tulimwambia hata waziri wa ujenzi kuhusiana na hili, akatueleza atalifanyia kazi suala hili na tunafahamu kuna maeneo mengi yenye uhitaji, lakini kwa Ukerewe hali yetu ni mbaya sana na Ukara kuna wananchi wengi wanaotumia huduma ya usafiri wa kivuko na tunaiomba serikali itusaidie njia ya (MV Ukara),” amesema Chang’ah.

Baadhi ya wakazi wa wilaya ya Ukerewe, wamesema kuwa hivi sasa wanalazimika kutumia usafiri wa mitumbwi kutoka kisiwa cha Ukara kwenda Bugogora kutokana na kuhofia kuzimika kwa vivuko hivyo vinavyomilikiwa na Wakala wa Huduma za Ufundi na Umeme (Temesa) mkoani hapa.

Mhandisi Ferdinand Mishamo, Meneja wa Temesa mkoa wa Mwanza, alipotafutwa ofisini kwake na Mtandao Huu, ili kuelezea hatua za matengenezo ya vivuko hivyo, hakuwa tayari kutoa ushirikiano wowote.

Wakazi wa Wilaya ya Ukerewe inayoundwa na visiwa vidogo 38, wanakabiliwa na changamoto ya vyombo vya usafiri wa majini, ambapo kwa sehemu kubwa wanategemea mitumbwi ya injini huku hali ya vivuko vya MV Ukara na MV Nyerere na yenyewe inatia shaka kutokana na injini zake kuzimika ghafla mara kwa mara kunakosababishwa na uchakavu.

error: Content is protected !!