August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

DC Mwanza amsweka rumande mwalimu

Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu

Spread the love

FRANCIS Chang’ah, Mkuu  wa Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, ameamuru Eladislaus mwalimu wa shule ya msingi ya Uhuru, awekwe rumande kwa muda usiofahamika kutokana na  kosa la kuwafungia darasani wanafunzi, anaandika Moses Mseti.

Imeelezwa kuwa, mwalimu huyo aliwafungia wanafunzi darasani siku ya jana mpaka saa mbili usiku, kwa kosa la kushindwa kujibu maswali ya hesabu za kuzidisha namba moja mpaka kumi na mbili maarufu kama “table”.

Amri ya DC wa Ukerewe kuwa mwalimu huyo awekwe rumande inatekelezwa ikiwa ni miezi miwili tangu Eliudi Mwaiteleke, Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, kumuamuru mwalimu mmoja kudeki vyoo vya wanafunzi baada ya kuvikuta ni vichafu.

DC Chang’ah alipata taarifa za kufungiwa kwa wanafunzi darasani kutoka kwa Husein Egobano Katibu wa UVCCM Wilaya ya Ukerewe, kwa njia ya simu, na baada ya hapo aliamuru Polisi wakamkamate mwalimu huyo na kumuweka rumande.

“Nilipewa taarifa za wanafunzi kufungiwa darasani na mwalimu. Nikaamua kufika shuleni hapo na kukuta ni kweli, ndipo nikaagiza polisi wamkamate mwalimu huyo na wamemuweka rumande kutokea jana mpaka sasa,” amesema.

DC huyo amesema kuwa, kitendo cha mwalimu kuwafungia wanafunzi mpaka usiku kilisababisha hofu na usumbufu mkubwa kwa wazazi na walezi walioanza kuwatafuta watoto wao sehemu mbalimbali za wilaya hiyo kwani si kawaida yao kutorejea nyumbani mapaka usiku.

error: Content is protected !!